0:00
0:00

Mlango 6

Kisha wana wa Israeli walifanya yaliyo maovu mbele za macho ya Bwana; Bwana akawatia mikononi mwa Midiani muda wa miaka saba
2 Mkono wa Midiani ulikuwa na nguvu juu ya Israeli; tena kwa sababu ya Midiani wana wa Israeli walijifanyia hayo mashimo yaliyo milimani, na hayo mapango, na hizo ngome.
3 Basi ikawa, hapo Israeli walipokuwa wamepanda mashamba, Wamidiani wakakwea, na Waamaleki, na hao wana wa mashariki; wakakwea juu yao;
4 wakapanga marago juu yao, na kuyaharibu hayo maongeo ya nchi, hata ufikapo Gaza, wala hawakuacha katika Israeli riziki ziwazo zote; kondoo, wala ng'ombe, wala punda.
5 Kwa maana walikwea na ng'ombe zao na hema zao, wakaja mfano wa nzige kwa wingi; wao na ngamia zao pia walikuwa hawana hesabu; nao waliingia katika hiyo nchi ili kuiharibu.
6 Israeli walitwezwa sana kwa sababu ya Wamidiani; nao wana wa Israeli wakamlilia Bwana.
7 Kisha ikawa, hapo wana wa Israeli walipomlilia Bwana kwa sababu ya Midiani,
8 Bwana akamtuma nabii aende kwa hao wana wa Israeli; naye akawaambia, Bwana, yeye Mungu wa Israeli, asema hivi, Mimi niliwaleta ninyi mkwee kutoka Misri, nikawatoa katika nyumba ya utumwa;
9 nami niliwaokoa na mikono ya Wamisri, na mikono ya wote waliokuwa wakiwaonea, nami niliwafukuza watoke mbele zenu, nami niliwapa ninyi nchi yao;
10 kisha niliwaambia, Mimi ndimi Bwana, Mungu wenu; msiiche miungu ya Waamori, ambayo mwaketi katika nchi yao; lakini hamkuitii sauti yangu.
11 Malaika wa Bwana akaenda akaketi chini ya mwaloni uliokuwa katika Ofra, uliokuwa mali yake Yoashi, Mwabiezeri; na mwanawe Gideoni alikuwa akipepeta ngano ndani ya shinikizo, ili kuificha machoni pa Wamidiani.
12 Malaika wa Bwana akamtokea, akamwambia, Bwana yu pamoja nawe, Ee shujaa.
13 Gideoni akamwambia, Ee Bwana wangu, ikiwa Bwana yu pamoja nasi, mbona mambo haya yote yametupata? Yako wapi matendo yake ya ajabu, waliyotuhadithia baba zetu, wakisema, Je! Siye Bwana, aliyetuleta huku kutoka Misri? Ila sasa ametutupa, naye ametutia katika mikono ya Midiani.
14 Bwana akamtazama, akasema, Enenda kwa uwezo wako huu, ukawaokoe Israeli na mkono wa Midiani. Je! Si mimi ninayekutuma?
15 Akamwambia, Ee Bwana, nitawaokoa Israeli kwa jinsi gani? Tazama, jamaa zangu ndio walio maskini sana katika Manase, na mimi ndimi niliye mdogo katika nyumba ya baba yangu.
16 Bwana akamwambia, Hakika nitakuwa pamoja nawe, nawe utawapiga Wamidiani kama mtu mmoja.
17 Naye akamwambia, Kama nimepata kibali mbele za macho yako, basi unionyeshe ishara, ya kuwa ndiwe wewe unayesema nami.
18 Tafadhali, usiondoke hapa hata nikujie, nikatoe zawadi yangu, na kuiweka mbele zako. Akasema, Nitangoja hata utakaporudi.
19 Basi Gideoni akaingia ndani, akaandaa mwana-mbuzi, na mikate isiyotiwa chachu, ya efa ya unga; akaitia ile nyama katika kikapu, akautia mchuzi katika nyungu, akamletea hapo nje chini ya mwaloni, akampa.
20 Naye malaika wa Mungu akamwambia, Itwae nyama na mikate isiyotiwa chachu, uiweke juu ya mwamba huu, ukaumwage huu mchuzi. Akafanya hivyo.
21 Ndipo malaika wa Bwana akanyosha ncha ya fimbo ile iliyokuwa mkononi mwake, akaigusa ile nyama na ile mikate; moto ukatoka mwambani, ukaiteketeza ile nyama na mikate; malaika wa Bwana akaondoka mbele ya macho yake.
22 Gideoni akaona ya kuwa ni malaika wa Bwana; Gideoni akasema, Ole wangu, Ee Bwana MUNGU! Kwa kuwa nimemwona Bwana uso kwa uso.
23 Bwana akamwambia Amani iwe pamoja nawe; usiogope; hutakufa.
24 Ndipo Gideoni akamjengea Bwana madhabahu hapo, akaiita jina lake, Yehova-Shalomu; hata hivi leo iko huko katika Ofra ya Waabiezeri.
25 Ikawa usiku uo huo Bwana akamwambia, Mtwae ng'ombe wa baba yako, yaani ng'ombe wa pili, wa miaka saba, ukaiangushe madhabahu ya Baali, aliyo nayo baba yako, ukaikate Ashera ile iliyo karibu nayo;
26 ukamjengee Bwana, Mungu wako, madhabahu juu ya ngome hii, kwa taratibu zake; ukamtwae yule ng'ombe wa pili na kumtoa awe sadaka ya kuteketezwa, kwa kuni za ile Ashera uliyoikata.
27 Ndipo Gideoni akatwaa watu kumi miongoni mwa watumishi wake, akafanya kama Bwana alivyomwambia; lakini ikawa kwa sababu aliwaogopa watu wa nyumba ya baba yake, na watu wa mji, hakuweza kuyatenda hayo wakati wa mchana, basi aliyatenda usiku.
28 Hata watu wa mji walipoondoka asubuhi na mapema, tazama, madhabahu ya Baali imebomolewa, na ile Ashera iliyokuwa karibu nayo imekatwa, na yule ng'ombe wa pili ametolewa sadaka juu ya ile madhabahu iliyojengwa.
29 Wakaambiana, Ni nani aliyetenda jambo hili? Hata walipotafuta habari na kuuliza, wakasema, Gideoni, mwana wa Yoashi, ndiye aliyetenda jambo hili.
30 Ndipo watu wa mji wakamwambia Yoashi Mlete mwanao, afe; kwa sababu ameibomoa madhabahu ya Baali na kwa sababu ameikata ile Ashera iliyokuwa karibu nayo.
31 Yoashi akawaambia watu wote waliokuwa wakishindana naye, Je! Mtamtetea Baali? Au mtamwokoa ninyi? Yeye atakayemtetea na auawe hivi asubuhi; kama yeye ni Mungu, na ajitetee nafsi yake, kwa sababu mtu mmoja ameibomoa madhabahu yake.
32 Basi akamwita Yerubaali siku hiyo, akisema, Baali na atete naye kwa ajili ya nafsi yake, kwa sababu ameibomoa madhabahu yake.
33 Wakati huo Wamidiani na Waamaleki, na hao wana wa mashariki walikutana pamoja; wakavuka na kupanga hema zao katika bonde la Yezreeli.
34 Lakini roho ya Bwana ikaja juu yake Gideoni; naye akapiga tarumbeta; na Abiezeri walikutanika na kumfuata.
35 Kisha akatuma wajumbe waende kati ya Manase yote; wao nao walikutana pamoja ili kumfuata; kisha akatuma wajumbe waende kwa Asheri, na kwa Zabuloni, na kwa Naftali; nao wakakwea ili kumlaki.
36 Gideoni akamwambia Mungu, Ikiwa wewe utawaokoa Israeli kwa mkono wangu, kama ulivyosema,
37 tazama, nitaweka ngozi ya kondoo katika kiwanja cha kupuria; na kama ukiwapo umande juu ya ngozi tu, na nchi yote ikiwa kavu, basi, hapo ndipo nitakapojua ya kuwa utawaokoa Israeli kwa mkono wangu, kama ulivyosema.
38 Ikawa hivyo; kwa maana aliondoka asubuhi na mapema, akaikamua ile ngozi, akautoa ule umande katika ile ngozi, bakuli zima la maji.
39 Gideoni akamwambia Mungu, Hasira yako isiwake juu yangu, nami nitasema mara hii tu; nakuomba, nijaribu kwa ngozi hii mara hii tu; sasa ngozi tu na iwe kavu, na uwe umande juu ya nchi yote.
40 Mungu akafanya hivyo usiku ule; maana ile ngozi tu ilikuwa kavu, napo palikuwa na umande juu ya nchi yote.