0:00
0:00

Mlango 16

Ndipo neno la Bwana likamjia Yehu mwana wa Hanani juu ya Baasha, kusema,
2 Kwa kuwa mimi nilikuinua kutoka katika mavumbi, na kukufanya uwe mkuu juu ya watu wangu Israeli; nawe umeiendea njia ya Yeroboamu, na kuwakosesha watu wangu Israeli, hata wanighadhibishe kwa makosa yao;
3 angalia, kuondoa nitawaondoa Baasha na jamaa yake; tena nitaifanya nyumba yako iwe kama nyumba ya Yeroboamu mwana wa Nebati.
4 Mtu amfiaye Baasha mjini mbwa watamla; naye amfiaye mashambani ndege wa angani watamla.
5 Basi, mambo yote ya Baasha yaliyosalia, na aliyoyafanya, na nguvu zake, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Israeli?
6 Baasha akalala na babaze, akazikwa katika Tirza; naye Ela mwanawe akatawala mahali pake.
7 Tena neno la Bwana likaja kwa mkono wa nabii Yehu mwana wa Hanani juu ya Baasha, na juu ya nyumba yake, kwa sababu ya mabaya yote aliyoyatenda machoni pa Bwana, akimghadhibisha kwa kazi ya mikono yake, kwa kufanana na nyumba ya Yeroboamu, na kwa sababu aliiharibu.
8 Katika mwaka wa ishirini na sita wa Asa mfalme wa Yuda, Ela mwana wa Baasha alianza kutawala juu ya Israeli huko Tirza, akatawala miaka miwili.
9 Na mtumwa wake Zimri, jemadari wa nusu ya magari yake, akamfanyia fitina; alipokuwako Tirza akinywa hata kulewa nyumbani mwa Arsa, aliyekuwa juu ya nyumba huko Tirza;
10 Zimri akaingia akampiga, akamwua, katika mwaka wa ishirini na saba wa Asa mfalme wa Yuda, akatawala mahali pake.
11 Ikawa, alipoanza kutawala, mara alipoketi juu ya kiti chake cha enzi, akawaua nyumba yote ya Baasha; hakumwachia mwanamume ye yote, wa jamaa zake, wala wa rafiki zake.
12 Hivyo Zimri akaiharibu nyumba yote ya Baasha, sawasawa na neno la Bwana, alilolinena juu ya Baasha kwa Yehu nabii,
13 kwa sababu ya makosa yake Baasha, na makosa yote ya Ela mwanawe, waliyoyakosa, na kuwakosesha Israeli, wakimghadhibisha Bwana, Mungu wa Israeli, kwa matendo yao ya ubatili.
14 Na mambo yote ya Ela yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Israeli?
15 Katika mwaka wa ishirini na saba wa Asa mfalme wa Yuda, Zimri akatawala muda wa siku saba huko Tirza. Basi, watu walikuwa wametua maragoni kupigana na Gibethoni, ulio wa Wafilisti.
16 Na hao watu waliokuwako maragoni wakasikia habari ya kwamba Zimri amefanya fitina, tena amempiga mfalme; kwa hiyo Israeli wote wakamfanya Omri, jemadari wa jeshi, awe mfalme juu ya Israeli siku ile maragoni.
17 Omri akapanda kutoka Gibethoni, na Israeli wote pamoja naye, wakauhusuru Tirza.
18 Ikawa Zimri alipoona ya kuwa mji umetwaliwa, akaingia ngomeni mwa nyumba ya mfalme, akaiteketeza nyumba ya mfalme juu yake kwa moto, akafa;
19 kwa sababu ya makosa aliyoyakosa, akifanya mabaya machoni pa Bwana, kwa kuiendea njia ya Yeroboamu na makosa yake aliyoyafanya akiwakosesha Israeli.
20 Na mambo yote ya Zimri yaliyosalia na fitina yake aliyoifanya, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Israeli?
21 Ndipo watu wa Israeli wakatengwa sehemu mbili; nusu ya watu wakamfuata Tibni mwana wa Ginathi, ili wamfanye mfalme; nusu wakamfuata Omri.
22 Lakini hao watu waliomfuata Omri wakawashinda watu waliomfuata Tibni mwana wa Ginathi; basi akafa Tibni, akatawala Omri.
23 Katika mwaka wa thelathini na moja wa Asa, mfalme wa Yuda, Omri alianza kutawala juu ya Israeli, akatawala miaka kumi na miwili. Akatawala huko Tirza miaka sita.
24 Kisha akanunua kilima cha Samaria kwa Shemeri kwa talanta mbili za fedha; akajenga juu ya kilima kile, akauita mji alioujenga Samaria, kwa kuliandama jina lake Shemeri, aliyekuwa mwenye kilima.
25 Omri akafanya yaliyo mabaya machoni pa Bwana, akatenda maovu kuliko wote waliomtangulia;
26 kwa kuwa aliiendea njia yote ya Yeroboamu mwana wa Nebati, na makosa yake, aliyowakosesha Israeli, ili kumghadhibisha Bwana, Mungu wa Israeli, kwa matendo yao ya ubatili.
27 Nayo mambo yote ya Omri yaliyosalia aliyoyatenda, na uthabiti alioufanya, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Israeli?
28 Omri akalala na babaze, akazikwa huko Samaria; na Ahabu mwanawe akatawala mahali pake.
29 Ahabu mwana wa Omri alianza kutawala juu ya Israeli katika mwaka wa thelathini na nane wa Asa mfalme wa Yuda; akatawala Ahabu mwana wa Omri juu ya Israeli katika Samaria miaka ishirini na miwili.
30 Ahabu mwana wa Omri akafanya yaliyo mabaya machoni pa Bwana kuliko wote waliomtangulia.
31 Ikawa, kama ingalikuwa neno dogo tu kuyaendea makosa ya Yeroboamu mwana wa Nebati, akamwoa Yezebeli binti Ethbaali, mfalme wa Wasidoni, akaenda akamtumikia Baali, akamsujudia.
32 Akamjengea Baali madhabahu katika nyumba ya Baali, aliyoijenga huko Samaria.
33 Ahabu akaifanya Ashera; Ahabu akazidi kumghadhibisha Bwana, Mungu wa Israeli, kuliko wafalme wote wa Israeli waliomtangulia.
34 Katika siku zake, Hieli Mbetheli akajenga Yeriko; akatia misingi yake kwa kufiwa na Abiramu mzaliwa wake wa kwanza, na kuyaweka malango yake kwa kufiwa na mwana wake mdogo Segubu; sawasawa na neno la Bwana alilolinena kwa Yoshua mwana wa Nuni.