0:00
0:00

Mlango 7

Ikawa baada ya mambo hayo, wakati wa kutawala kwake Artashasta, mfalme wa Uajemi, Ezra, mwana wa Seraya, mwana wa Azaria, mwana wa Hilkia,
2 mwana wa Shalumu, mwana wa Sadoki, mwana wa Ahitubu,
3 mwana wa Amaria, mwana wa Azaria, mwana wa Merayothi,
4 mwana wa Zerahia, mwana wa Uzi, mwana wa Buki,
5 mwana wa Abishua, mwana wa Finehasi, mwana wa Eleazari, mwana wa Haruni, kuhani mkuu;
6 huyo Ezra akakwea kutoka Babeli; naye alikuwa mwandishi mwepesi katika sheria ya Musa, aliyokuwa ameitoa Bwana, Mungu wa Israeli; naye mfalme akamjalia matakwa yake yote, kama mkono wa Bwana, Mungu wake, ulivyokuwa pamoja naye.
7 Nao wakakwea baadhi ya wana wa Israeli, na wa makuhani, na wa Walawi, na waimbaji, na mabawabu, na Wanethini, ili kwenda Yerusalemu, katika mwaka wa saba wa mfalme Artashasta.
8 Naye Ezra akafika Yerusalemu mwezi wa tano katika mwaka wa saba wa huyo mfalme.
9 Maana alianza kukwea kutoka Babeli siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza, naye akafika Yerusalemu siku ya kwanza ya mwezi wa tano, kama mkono mwema wa Mungu wake ulivyokuwa pamoja naye.
10 Kwa maana huyo Ezra alikuwa ameuelekeza moyo wake kuitafuta sheria ya Bwana, na kuitenda, na kufundisha maagizo na hukumu katika Israeli.
11 Basi hii ndiyo nakala ya waraka, mfalme Artashasta aliyompa Ezra, kuhani, mwandishi, naam, mwandishi wa maneno ya amri za Bwana, na wa sheria zake alizowapa Israeli.
12 Artashasta, mfalme wa wafalme, kwa Ezra, kuhani, mwandishi wa torati ya Mungu wa mbinguni, salamu kamili; wakadhalika.
13 Natoa amri ya kwamba wote walio wa watu wa Israeli, na makuhani wao, na Walawi, katika ufalme wangu, wenye nia ya kwenda Yerusalemu kwa hiari yao wenyewe, waende pamoja nawe.
14 Kwa kuwa umetumwa na mfalme, na washauri wake saba, ili kuuliza habari za Yuda na Yerusalemu, kwa sheria ya Mungu wako iliyo mkononi mwako;
15 na kuichukua fedha na dhahabu, ambayo mfalme, na washauri wake, kwa hiari yao, wamemtolea Mungu wa Israeli, akaaye Yerusalemu;
16 na fedha yote na dhahabu utakayoona katika wilaya ya Babeli, pamoja na vitu watakavyotoa watu kwa hiari yao, na vitu vya makuhani walivyotoa kwa hiari yao, kwa ajili ya nyumba ya Mungu wao iliyoko Yerusalemu.
17 Kwa sababu hiyo ujitahidi kununua kwa fedha hiyo mafahali, kondoo waume, wana-kondoo, pamoja na sadaka zao za unga, na sadaka zao za kinywaji; nawe utazitoa juu ya madhabahu ya nyumba ya Mungu wenu, iliyoko Yerusalemu.
18 Na neno lo lote mtakaloona vema kulitenda, wewe na ndugu zako, kwa ile fedha na dhahabu itakayobaki, hilo litendeni, kama apendavyo Mungu wenu.
19 Na vile vyombo upewavyo kwa huduma ya nyumba ya Mungu wako, virejeze mbele za Mungu wa Yerusalemu.
20 Na cho chote kitakachohitajiwa zaidi, kwa ajili ya nyumba ya Mungu wako, kitakachokupasa kukitoa, kitoe katika nyumba ya hazina ya mfalme.
21 Na mimi, naam mimi, mfalme Artashasta, nawapa amri wote wenye kutunza hazina, walio ng'ambo ya Mto, ya kwamba, kila neno ambalo Ezra, kuhani, mwandishi wa torati ya Mungu wa mbinguni, atalitaka kwenu, na litendeke kwa bidii nyingi,
22 hata kiasi cha talanta mia za fedha, na vipimo mia vya ngano, na bathi mia za divai, na bathi mia za mafuta, na chumvi bila kuuliza kiasi chake.
23 Kila neno litakaloamriwa na Mungu wa mbinguni, na litendeke halisi kwa ajili ya nyumba ya Mungu wa mbinguni. Kwa nini itokee ghadhabu juu ya ufalme wa mfalme na wanawe?
24 Tena twawaarifuni ya kuwa katika habari ya makuhani, na Walawi, na waimbaji, na mabawabu na Wanethini, au watumishi wa nyumba hii ya Mungu, si halali kuwatoza kodi, wala ada, wala ushuru.
25 Na wewe, Ezra, kwa kadiri ya hekima ya Mungu wako iliyo mkononi mwako, waweke waamuzi na makadhi, watakaowahukumu watu wote walio ng'ambo ya Mto, yaani, wote wenye kuzijua amri za Mungu wako; ukamfundishe yeye asiyezijua.
26 Na kila mtu asiyekubali kuitenda sheria ya Mungu wako, na sheria ya mfalme, na apatilizwe hukumu kwa bidii, kwamba ni kuuawa, au kwamba ni kuhamishwa, au kuondolewa mali yake, au kufungwa.
27 Na ahimidiwe Bwana, Mungu wa baba zetu, aliyetia neno kama hilo katika moyo wa mfalme, kuipamba nyumba ya Bwana iliyoko Yerusalemu.
28 Naye amenifikilizia rehema zake mbele ya mfalme, na washauri wake, na mbele ya wakuu wote wa mfalme wenye mamlaka. Nami nikatiwa nguvu, kwa kadiri mkono wa Bwana, Mungu wangu, ulivyokuwa pamoja nami, nikawakusanya wakuu wote katika Israeli, ili wakwee pamoja nami.