0:00
0:00

Mlango 6

Njoni, tumrudie Bwana; maana yeye amerarua, na yeye atatuponya; yeye amepiga, na yeye atatufunga jeraha zetu.
2 Baada ya siku mbili atatufufua; siku ya tatu atatuinua, nasi tutaishi mbele zake.
3 Nasi na tujue, naam, tukaendelee kumjua Bwana; kutokea kwake ni yakini kama asubuhi; naye atatujilia kama mvua, kama mvua ya vuli iinyweshayo nchi.
4 Ee Efraimu, nikutendee nini? Ee Yuda, nikutendee nini? Kwa maana fadhili zenu ni kama wingu la asubuhi na kama umande utowekao mapema.
5 Kwa sababu hiyo nimewakata-kata kwa vinywa vya manabii; nimewaua kwa maneno ya kinywa changu; na hukumu yangu itatokea kama mwanga.
6 Maana nataka fadhili wala si sadaka; na kumjua Mungu kuliko sadaka za kuteketezwa.
7 Lakini wao wamelivunja hilo agano kama Adamu; huko wamenitenda mambo ya hiana.
8 Gileadi ni mji wa hao watendao maovu, umetiwa rangi ya damu.
9 Na kama vile makundi ya wanyang'anyi wamwoteavyo mtu, ndivyo kundi la makuhani wauavyo katika njia ielekeayo Shekemu; naam, wametenda mambo maovu sana.
10 Katika nyumba ya Israeli nimeona jambo bovu kabisa; huko uzinzi umeonekana katika Efraimu; Israeli ametiwa unajisi.
11 Tena, Ee Yuda, wewe umeandikiwa mavuno, hapo nitakapowarudisha wafungwa wa watu wangu.