Yona

1 2 3 4

0:00
0:00

Mlango 2

Ndipo Yona akamwomba Bwana, Mungu wake, katika tumbo la yule samaki,
2 Akasema, Nalimlilia Bwana kwa sababu ya shida yangu, Naye akaniitikia; Katika tumbo la kuzimu naliomba, Nawe ukasikia sauti yangu.
3 Maana ulinitupa vilindini, Ndani ya moyo wa bahari; Gharika ya maji ikanizunguka pande zote; Mawimbi yako yote na gharika zako zote zimepita juu yangu.
4 Nami nikasema, Nimetupwa mbali na macho yako; Lakini nitatazama tena kukabili hekalu lako takatifu.
5 Maji yalinizunguka, hata nafsini mwangu; Vilindi vilinizunguka; Mwani ulikizinga kichwa changu;
6 Nalishuka hata pande za chini za milima; Hiyo nchi na mapingo yake yalinifunga hata milele; Lakini umeipandisha nafsi yangu kutoka shimoni, Ee Bwana, Mungu wangu,
7 Roho yangu ilipozimia ndani yangu, Nalimkumbuka Bwana; Maombi yangu yakakuwasilia, Katika hekalu lako takatifu.
8 Watu waangaliao mambo ya ubatili na uongo Hujitenga na rehema zao wenyewe;
9 Lakini mimi nitakutolea sadaka kwa sauti ya shukrani; Nitaziondoa nadhiri zangu. Wokovu hutoka kwa Bwana.
10 Bwana akasema na yule samaki, naye akamtapika Yona pwani.