0:00
0:00

Mlango 9

Akawaambia, Amin, nawaambia, Pana watu katika hawa wasimamao hapa, ambao hawataonja mauti kabisa, hata watakapouona ufalme wa Mungu umekuja kwa nguvu.
2 Hata baada ya siku sita Yesu akawatwaa Petro, na Yakobo, na Yohana, akawaleta juu ya mlima mrefu faraghani, peke yao; akageuka sura yake mbele yao;
3 mavazi yake yakimeta-meta, meupe mno, jinsi asivyoweza dobi duniani kuyafanya meupe.
4 Wakatokewa na Eliya pamoja na Musa, nao walikuwa wakizungumza na Yesu.
5 Petro akajibu, akamwambia Yesu, Rabi, ni vizuri sisi kuwapo hapa; na tufanye vibanda vitatu, kimoja chako wewe, kimoja cha Musa, na kimoja cha Eliya.
6 Maana, hakujua la kunena, kwa kuwa waliingiwa na hofu nyingi.
7 Kisha likatokea wingu, likawatia uvuli; sauti ikatoka katika lile wingu, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, msikieni yeye.
8 Mara hiyo walipotazama huku na huku, hawakuona mtu pamoja nao ila Yesu peke yake.
9 Na walipokuwa wakishuka mlimani aliwakataza wasimweleze mtu waliyoyaona, hata Mwana wa Adamu atakapokuwa amefufuka katika wafu.
10 Wakalishika neno lile, wakiulizana wao kwa wao, Huko kufufuka katika wafu maana yake nini?
11 Wakamwuliza, wakisema, Mbona waandishi hunena ya kwamba imempasa Eliya kuja kwanza?
12 Akajibu akawaambia, Ni kweli Eliya yuaja kwanza, na kurejeza upya yote; lakini, pamoja na haya, ameandikiwaje Mwana wa Adamu ya kwamba atateswa mengi na kudharauliwa?
13 Lakini nawaambia, Eliya amekwisha kuja, nao wakamtenda yote waliyoyataka kama alivyoandikiwa.
14 Hata walipowafikia wanafunzi, waliona mkutano mkuu wakiwazunguka, na waandishi wakijadiliana nao;
15 mara mkutano wote walipomwona walishangaa, wakamwendea mbio, wakamsalimu.
16 Akawauliza, Mnajadiliana nini nao?
17 Mtu mmoja katika mkutano akamjibu, Mwalimu, nimemleta mwanangu kwako, ana pepo bubu;
18 na kila ampagaapo, humbwaga chini, naye hutoka povu na kusaga meno na kukonda; nikasema na wanafunzi wako wamtoe pepo, wasiweze.
19 Akawajibu, akasema, Enyi kizazi kisichoamini, nikae nanyi hata lini? Nichukuliane nanyi hata lini? Mleteni kwangu.
20 Wakamleta kwake; hata alipomwona, mara yule pepo alimtia kifafa; naye akaanguka chini, akagaa-gaa, akitokwa na povu.
21 Akamwuliza babaye, Amepatwa na haya tangu lini? Akasema, Tangu utoto.
22 Na mara nyingi amemtupa katika moto, na katika maji, amwangamize; lakini ukiweza neno lo lote, utuhurumie, na kutusaidia.
23 Yesu akamwambia, Ukiweza! Yote yawezekana kwake aaminiye.
24 Mara babaye yule kijana akapaza sauti, akasema, Naamini, nisaidie kutokuamini kwangu.
25 Naye Yesu akiona ya kuwa mkutano unakusanyika mbio, akamkemea yule pepo mchafu, akamwambia, Ewe pepo bubu na kiziwi, mimi nakuamuru, mtoke huyu, wala usimwingie tena.
26 Akalia, akamtia kifafa sana, akamtoka; naye akawa kama amekufa; hata wengi wakasema, Amekufa.
27 Lakini Yesu akamshika mkono akamwinua naye akasimama.
28 Hata alipoingia nyumbani, wanafunzi wake wakamwuliza kwa faragha, Mbona sisi hatukuweza kumtoa?
29 Akawaambia, Namna hii haiwezi kutoka kwa neno lo lote, isipokuwa kwa kuomba.
30 Wakatoka huko, wakapita katikati ya Galilaya; naye hakutaka mtu kujua.
31 Kwa sababu alikuwa akiwafundisha wanafunzi wake, akawaambia, Mwana wa Adamu yuaenda kutiwa katika mikono ya watu, nao watamwua; hata akiisha kuuawa, baada ya siku tatu atafufuka.
32 Lakini hawakulifahamu neno lile, wakaogopa kumwuliza.
33 Wakafika Kapernaumu; hata alipokuwamo nyumbani, akawauliza, Mlishindania nini njiani?
34 Wakanyamaza; kwa maana njiani walikuwa wakibishana wao kwa wao, ni nani aliye mkubwa.
35 Akaketi chini, akawaita wale Thenashara akawaambia, Mtu atakaye kuwa wa kwanza atakuwa wa mwisho kuliko wote, na mtumishi wa wote.
36 Akatwaa kitoto, akamweka katikati yao, akamkumbatia, akawaambia,
37 Mtu akimpokea mtoto mmoja wa namna hii kwa jina langu, anipokea mimi; na mtu akinipokea mimi, humpokea, si mimi, bali yeye aliyenituma.
38 Yohana akamjibu, akamwambia, Mwalimu, tulimwona mtu akitoa pepo kwa jina lako, ambaye hafuatani nasi; tukamkataza, kwa sababu hafuatani nasi.
39 Yesu akasema, Msimkataze, kwa kuwa hakuna mtu atakayefanya mwujiza kwa jina langu akaweza mara kuninenea mabaya;
40 kwa sababu asiye kinyume chetu, yu upande wetu.
41 Kwa kuwa ye yote atakayewanywesha ninyi kikombe cha maji, kwa kuwa ninyi ni watu wa Kristo, amin, nawaambia, hatakosa thawabu yake.
42 Na ye yote atakayemkosesha mmojawapo wa wadogo hawa waniaminio, afadhali afungiwe jiwe la kusagia shingoni mwake, na kutupwa baharini.
43 Na mkono wako ukikukosesha, ukate; ni afadhali kuingia katika uzima u kigutu, kuliko kuwa na mikono miwili, na kwenda zako jehanum, kwenye moto usiozimika;
44 ambamo humo funza wao hafi, wala moto hauzimiki.
45 Na mguu wako ukikukosesha, ukate; ni afadhali kuingia katika uzima, u kiwete, kuliko kuwa na miguu miwili, na kutupwa katika jehanum;
46 ambamo humo funza wao hafi, wala moto hauzimiki.
47 Na jicho lako likikukosesha, ling'oe, ulitupe; ni afadhali kuingia katika ufalme wa Mungu, una chongo, kuliko kuwa na macho mawili, na kutupwa katika jehanum;
48 ambamo humo funza wao hafi, wala moto hauzimiki.
49 Kwa sababu kila mtu atatiwa chumvi kwa moto.
50 Chumvi ni njema; lakini chumvi ikiwa si chumvi tena, mtaitia nini ikolee? Mwe na chumvi ndani yenu, mkakae kwa amani ninyi kwa ninyi.