0:00
0:00

Mlango 15

Basi watoza ushuru wote na wenye dhambi walikuwa wakimkaribia wamsikilize.
2 Mafarisayo na waandishi wakanung'unika, wakisema, Mtu huyu huwakaribisha wenye dhambi, tena hula nao.
3 Akawaambia mfano huu, akisema,
4 Ni nani kwenu, mwenye kondoo mia, akipotewa na mmojawapo, asiyewaacha wale tisini na kenda nyikani, aende akamtafute yule aliyepotea hata amwone?
5 Naye akiisha kumwona, humweka mabegani pake akifurahi.
6 Na afikapo nyumbani kwake, huwaita rafiki zake na jirani zake, akawaambia, Furahini pamoja nami, kwa kuwa nimekwisha kumpata kondoo wangu aliyepotea.
7 Nawaambia, Vivyo hivyo kutakuwa na furaha mbinguni kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye, kuliko kwa ajili ya wenye haki tisini na kenda ambao hawana haja ya kutubu.
8 Au kuna mwanamke gani mwenye shilingi kumi, akipotewa na moja, asiyewasha taa na kufagia nyumba, na kutafuta kwa bidii hata aione?
9 Na akiisha kuiona, huwaita rafiki zake na jirani zake, akawaambia, Furahini pamoja nami, kwa kuwa nimeipata tena shilingi ile iliyonipotea.
10 Nawaambia, Vivyo hivyo kuna furaha mbele ya malaika wa Mungu kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye.
11 Akasema, Mtu mmoja alikuwa na wana wawili;
12 yule mdogo akamwambia babaye, Baba, nipe sehemu ya mali inayoniangukia. Akawagawia vitu vyake.
13 Hata baada ya siku si nyingi, yule mdogo akakusanya vyote, akasafiri kwenda nchi ya mbali; akatapanya mali zake huko kwa maisha ya uasherati.
14 Alipokuwa amekwisha tumia vyote, njaa kuu iliingia nchi ile, yeye naye akaanza kuhitaji.
15 Akaenda akashikamana na mwenyeji mmoja wa nchi ile; naye alimpeleka shambani kwake kulisha nguruwe.
16 Akawa akitamani kujishibisha kwa maganda waliyokula nguruwe, wala hapana mtu aliyempa kitu.
17 Alipozingatia moyoni mwake, alisema, Ni watumishi wangapi wa baba yangu wanaokula chakula na kusaza, na mimi hapa ninakufa kwa njaa.
18 Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu na kumwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako;
19 sistahili kuitwa mwana wako tena; nifanye kama mmoja wa watumishi wako.
20 Akaondoka, akaenda kwa babaye. Alipokuwa angali mbali, baba yake alimwona, akamwonea huruma, akaenda mbio akamwangukia shingoni, akambusu sana.
21 Yule mwana akamwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako; sistahili kuitwa mwana wako tena.
22 Lakini baba aliwaambia watumwa wake, Lileteni upesi vazi lililo bora, mkamvike; mtieni na pete kidoleni, na viatu miguuni;
23 mleteni ndama yule aliyenona mkamchinje; nasi tule na kufurahi;
24 kwa kuwa huyu mwanangu alikuwa amekufa, naye amefufuka; alikuwa amepotea, naye ameonekana. Wakaanza kushangilia.
25 Basi, yule mwanawe mkubwa alikuwako shamba na alipokuwa akija na kuikaribia nyumba, alisikia sauti ya nyimbo na machezo.
26 Akaita mtumishi mmoja, akamwuliza, Mambo haya, maana yake nini?
27 Akamwambia, Ndugu yako amekuja, na baba yako amemchinja ndama aliyenona, kwa sababu amempata tena, yu mzima.
28 Akakasirika, akakataa kuingia ndani. Basi babaye alitoka nje, akamsihi.
29 Akamjibu baba yake, akasema, Tazama, mimi nimekutumikia miaka mingapi hii, wala sijakosa amri yako wakati wo wote, lakini hujanipa mimi mwana-mbuzi, nifanye furaha na rafiki zangu;
30 lakini, alipokuja huyu mwana wako aliyekula vitu vyako pamoja na makahaba, umemchinjia yeye ndama aliyenona.
31 Akamwambia, Mwanangu, wewe u pamoja nami sikuzote, na vyote nilivyo navyo ni vyako.
32 Tena, kufanya furaha na shangwe ilipasa, kwa kuwa huyu ndugu yako alikuwa amekufa, naye amefufuka; alikuwa amepotea, naye ameonekana.