0:00
0:00

Mlango 112

Haleluya. Heri mtu yule amchaye Bwana, Apendezwaye sana na maagizo yake.
2 Wazao wake watakuwa hodari duniani; Kizazi cha wenye adili kitabarikiwa.
3 Nyumbani mwake mna utajiri na mali, Na haki yake yakaa milele.
4 Nuru huwazukia wenye adili gizani; Ana fadhili na huruma na haki.
5 Heri atendaye fadhili na kukopesha; Atengenezaye mambo yake kwa haki.
6 Kwa maana hataondoshwa kamwe; Mwenye haki atakumbukwa milele.
7 Hataogopa habari mbaya; Moyo wake u imara ukimtumaini Bwana.
8 Moyo wake umethibitika hataogopa, Hata awaone watesi wake wameshindwa.
9 Amekirimu, na kuwapa maskini, Haki yake yakaa milele, Pembe yake itatukuzwa kwa utukufu.
10 Asiye haki ataona na kusikitika, Atasaga meno yake na kuyeyuka, Tamaa ya wasio haki itapotea.