0:00
0:00

Mlango 14

Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
2 Hii ndiyo sheria ya mwenye ukoma, katika siku ya kutakaswa kwake; ataletwa kwa kuhani,
3 na huyo kuhani atatoka aende nje ya marago; na kuhani ataangalia, na tazama, ikiwa pigo la ukoma limepoa kwake huyo mwenye ukoma;
4 ndipo huyo kuhani ataagiza kwamba watwae kwa ajili yake atakayetakaswa ndege wawili walio hai, ambao ni safi, na mti wa mwerezi, na sufu nyekundu, na hisopo;
5 kisha kuhani ataagiza ndege mmoja achinjwe katika chombo cha udongo kilicho juu ya maji ya mtoni;
6 kisha huyo ndege aliye hai atamshika, na huo mti wa mwerezi, na hiyo sufu nyekundu, na hisopo, naye atavichovya hivyo, pamoja na yule ndege aliye hai, katika damu ya huyo ndege aliyechinjwa juu ya maji ya mtoni;
7 kisha atamnyunyizia huyo atakayetakaswa na ukoma mara saba, naye atasema kwamba yu safi, kisha atamwacha yule ndege aliye hai aende zake nyikani.
8 Naye huyo atakayetakaswa atazifua nguo zake, na kunyoa nywele zake zote, na kuoga katika maji, naye atakuwa safi; baada ya hayo ataingia ndani ya marago, lakini ataketi nje ya hema yake muda wa siku saba.
9 Kisha siku ya saba atanyoa nywele zote za kichwani mwake, na ndevu zake, na nyushi zake, nywele zake zote pia atazinyoa; kisha atazifua nguo zake, na kuoga mwili wake majini, naye atakuwa safi.
10 Kisha siku ya nane atachukua wana-kondoo wawili waume wakamilifu, na mwana-kondoo mmoja wa kike wa mwaka wa kwanza mkamilifu, na sehemu tatu za kumi za efa moja ya unga mwembamba kuwa sadaka ya unga, kuchanganywa na mafuta, na logi moja ya mafuta.
11 Kisha kuhani atakayemtakasa atamsimamisha huyo mtu atakayetakaswa, pamoja na vitu vile vyote, mbele za Bwana, mlangoni pa hema ya kukutania;
12 kisha kuhani atamshika mmoja katika hao wana-kondoo waume, na kumsongeza awe sadaka ya hatia, pamoja na hiyo logi ya mafuta, kisha atavitikisa kuwa ni sadaka ya kutikiswa mbele za Bwana;
13 kisha atamchinja huyo mwana-kondoo mahali hapo wachinjapo sadaka ya dhambi na sadaka ya kuteketezwa, ndani ya mahali patakatifu; kwa kuwa kama hiyo sadaka ya dhambi ilivyo ya kuhani, ni vivyo sadaka ya hatia; ni takatifu sana;
14 kisha huyo kuhani atatwaa katika hiyo damu ya sadaka ya hatia, naye kuhani ataitia katika ncha ya sikio la kuume la huyo atakayetakaswa, na katika chanda cha gumba cha mkono wake wa kuume, na katika kidole kikuu cha mguu wake wa kuume;
15 kisha kuhani atatwaa katika hiyo logi ya mafuta, na kuyamimina katika kitanga cha mkono wake mwenyewe wa kushoto;
16 kisha kuhani atatia kidole cha mkono wa kuume katika hayo mafuta, yaliyo katika mkono wake wa kushoto, naye atayanyunyiza hayo mafuta kwa kidole chake mara saba mbele za Bwana;
17 na katika yale mafuta yaliyobaki mkononi mwake kuhani atayatia katika ncha ya sikio la kuume la huyo atakayetakaswa, na katika chanda cha gumba cha mkono wake wa kuume, na katika kidole kikuu cha mguu wake wa kuume, juu ya damu ya sadaka ya hatia;
18 na mafuta yaliyobaki, yaliyo katika mkono wa kuhani, atayatia juu ya kichwa cha huyo atakayetakaswa; na kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake, mbele za Bwana.
19 Kisha kuhani atasongeza sadaka ya dhambi, na kufanya upatanisho kwa ajili yake huyo atakayetakaswa kwa sababu ya unajisi wake; kisha baadaye ataichinja sadaka ya kuteketezwa;
20 kisha kuhani ataisongeza hiyo sadaka ya kuteketezwa, na sadaka ya unga, juu ya madhabahu na kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake, naye atakuwa safi.
21 Tena kwamba ni maskini, naye hawezi kupata kiasi hicho, ndipo atatwaa mwana-kondoo mmoja wa kiume, awe sadaka ya hatia ya kutikiswa, ili kufanya upatanisho kwa ajili yake, na sehemu ya kumi ya efa ya unga mwembamba, uliochanganywa na mafuta kuwa sadaka ya unga, na logi ya mafuta;
22 na hua wawili, au makinda mawili ya njiwa, kama awezavyo kuwapata; huyo mmoja atakuwa sadaka ya dhambi, na wa pili atakuwa sadaka ya kuteketezwa.
23 Hata siku ya nane atawaleta kwa kuhani, mlangoni pa hema ya kukutania mbele za Bwana, kwa ajili ya kutakaswa kwake.
24 Na kuhani atamtwaa huyo mwana-kondoo wa sadaka ya hatia, na hiyo logi ya mafuta, naye kuhani atavitikisa viwe sadaka ya kutikiswa mbele za Bwana;
25 kisha atamchinja mwana-kondoo wa sadaka ya hatia, na kuhani atatwaa katika damu ya sadaka ya hatia, na kuitia katika ncha ya sikio la kuume la huyo atakayetakaswa, na katika chanda cha gumba cha mkono wake wa kuume, na katika kidole kikuu cha mguu wake wa kuume;
26 kisha kuhani atamimina sehemu ya hayo mafuta katika kitanga cha mkono wake mwenyewe wa kushoto;
27 kisha kuhani atanyunyiza baadhi ya hayo mafuta yaliyo katika mkono wake wa kushoto, kwa kidole chake cha mkono wa kuume mara saba mbele za Bwana;
28 kisha kuhani atatia mengine katika hayo mafuta yaliyo mkononi mwake katika ncha ya sikio la kuume la huyo atakayetakaswa, na katika chanda cha gumba cha mkono wake wa kuume, na katika kidole kikuu cha mguu wake wa kuume, juu ya mahali pale penye damu ya sadaka ya hatia;
29 na mafuta yaliyobaki katika mkono wa kuhani atayatia juu ya kichwa cha huyo atakayetakaswa, ili kufanya upatanisho kwa ajili yake mbele za Bwana.
30 Kisha atasongeza hao hua mmojawapo, au hao makinda ya njiwa mmojawapo, kadiri ya awezao kuwapata;
31 hata kadiri aliyoweza, mmoja kuwa sadaka ya dhambi, na wa pili kuwa sadaka ya kuteketezwa, pamoja na sadaka ya unga; na huyo kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake huyo atakayetakaswa mbele za Bwana.
32 Huyo ambaye ndani yake mna pigo la ukoma, ambaye hawezi kukipata hicho kipasacho kutakaswa kwake, sheria yake ni hiyo.
33 Bwana akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia,
34 Hapo mtakapoingia nchi ya Kanaani, ambayo nawapa kuwa ni milki yenu, nami nitakapolitia pigo la ukoma katika nyumba ya nchi hiyo ya milki yenu;
35 ndipo mwenye nyumba hiyo atakwenda na kumwambia kuhani, akisema, Naona mimi ya kwamba pana kama pigo katika nyumba yangu;
36 ndipo kuhani ataagiza kwamba watoe vyote vilivyomo nyumbani, mbele ya kuhani hajaingia ndani kuliangalia hilo pigo, ili kwamba vyote vilivyomo nyumbani visiwekwe kuwa unajisi; kisha baadaye kuhani ataingia ndani ya nyumba hiyo aitazame;
37 naye ataliangalia hilo pigo, na tazama, likiwa pigo limo ndani ya kuta za nyumba, nalo lina mashimo-mashimo, rangi ya majani, au mekundu, na kuonekana kuingia ndani kuliko huo ukuta;
38 ndipo kuhani atatoka katika nyumba hiyo mpaka mlangoni pa nyumba, na kuifunga hiyo nyumba muda wa siku saba;
39 siku ya saba kuhani atakwenda tena, naye ataangalia; na tazama, likiwa pigo limeenea katika kuta za nyumba;
40 ndipo kuhani atawaambia wayatoe hayo mawe, yaliyo na pigo, na kuyatupa mahali penye uchafu nje ya mji;
41 naye atafanya kwamba hiyo nyumba ikwanguwe ndani pande zote, na chokaa watakayokwangua wataimwaga nje ya mji mahali palipo na uchafu;
42 kisha watatwaa mawe mengine, na kuyatia mahali pa mawe hayo; naye atatwaa chokaa nyingine, na kuipaka chokaa hiyo nyumba.
43 Na kama hilo pigo likirudi tena, na kutokea ndani ya nyumba, baada ya yeye kuyatoa hayo mawe, na baada ya kuikwangua nyumba, na baada ya kupakwa chokaa,
44 ndipo kuhani ataingia ndani na kuangalia, na tazama, likiwa pigo limeenea ndani ya hiyo nyumba, ni ukoma unaokula hiyo nyumba; ni katika unajisi.
45 Naye ataibomoa nyumba, mawe yake, na miti yake, na chokaa yote ya hiyo nyumba; naye atavichukua vyote nje ya mji hata mahali palipo na uchafu.
46 Tena mtu atakayeingia ndani ya hiyo nyumba wakati huo wote iliofungwa, atakuwa najisi hata jioni.
47 Na mtu alalaye ndani ya nyumba hiyo atazifua nguo zake, naye alaye chakula ndani ya nyumba hiyo atazifua nguo zake.
48 Tena kwamba kuhani akiingia ndani na kuangalia, na tazama, ikiwa pigo halikuenea katika hiyo nyumba, baada ya nyumba kupakwa chokaa; ndipo kuhani atasema kwamba hiyo nyumba i safi, maana, pigo limepoa.
49 Naye atatwaa ndege wawili, na mti wa mwerezi, na sufu nyekundu, na hisopo, kwa kuitakasa hiyo nyumba;
50 naye atamchinja mmojawapo wa ndege hao katika chombo cha udongo kilicho juu ya maji ya mtoni;
51 kisha atatwaa huo mti wa mwerezi, na hisopo, na sufu nyekundu, pamoja na huyo ndege aliye hai, na kuvichovya vyote katika damu ya huyo ndege aliyechinjwa, na katika hayo maji ya mtoni, na kuinyunyiza nyumba mara saba;
52 naye ataitakasa hiyo nyumba kwa damu ya ndege, na kwa maji ya mtoni, na kwa huyo ndege aliye hai, na kwa mti wa mwerezi, na kwa hisopo, na kwa sufu nyekundu;
53 lakini ndege aliye hai atamwacha atoke mle mjini aende nyikani; ndivyo atakavyofanya upatanisho kwa ajili ya hiyo nyumba; nayo itakuwa safi.
54 Hiyo ndiyo sheria ya pigo la ukoma ya kila aina, na ya kipwepwe;
55 na ya ukoma wa vazi, na ukoma wa nyumba;
56 na kivimbe, na kikoko na kipaku king'aacho;
57 ili kufunza itakapokuwa ni unajisi, na itakapokuwa ni safi; hiyo ndiyo sheria ya ukoma.