0:00
0:00

Mlango 25

Kisha Bwana akanena na Musa katika mlima wa Sinai, na kumwambia,
2 Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Hapo mtakapoingia katika nchi niwapayo, ndipo hiyo nchi itashika Sabato kwa ajili ya Bwana.
3 Panda shamba lako miaka sita, na miaka sita lipelee shamba lako la mizabibu, na kuyachuma matunda yake;
4 lakini katika mwaka wa saba itakuwa ni Sabato ya kustarehe kabisa kwa ajili ya hiyo nchi, ni Sabato kwa Bwana; usipande shamba lako, wala usipelee shamba lako la mizabibu.
5 Hicho kimeacho chenyewe katika mavuno yako, usikivune, wala zabibu za mizabibu isiyopelewa usizitunde; utakuwa mwaka wa kustarehe kabisa kwa ajili ya hiyo nchi.
6 Na hiyo Sabato ya nchi itakuwa chakula kwenu; kwako wewe, na kwa mtumwa wako, na kwa mjakazi wako, na kwa mtumishi aliyeajiriwa, na kwa mgeni wako akaaye pamoja nawe;
7 na kwa hayawani wako, na kwa wanyama walio katika nchi yako; maongeo yote yatakuwa ni chakula chao.
8 Nawe utajihesabia Sabato saba za miaka, maana, miaka saba mara saba; zitakuwa ni siku za Sabato saba za miaka kwenu, maana miaka arobaini na kenda.
9 Ndipo utakapoipeleka pande zote hiyo baragumu yenye sauti kuu, siku ya kumi ya mwezi wa saba; katika siku hiyo ya upatanisho mtaipeleka baragumu katika nchi yenu yote.
10 Na mwaka wa hamsini mtautakasa, na kupiga mbiu ya kuachwa mahuru katika nchi yote kwa watu wote wanayokaa; itakuwa ni yubile kwenu, nanyi kila mtu atairudia milki yake mwenyewe, nanyi mtarejea kila mtu kwa jamaa yake.
11 Mwaka huo wa hamsini utakuwa ni yubile kwenu; msipande mbegu, wala msivune kitu hicho kimeacho chenyewe, wala msizitunde zabibu za mizabibu isiyopelewa.
12 Kwa kuwa ni yubile; utakuwa mwaka mtakatifu kwenu; mtakula maongeo yake yatokayo shambani.
13 Mwaka huo wa yubile mtairudia kila mtu milki yake.
14 Tena kama ukimwuzia jirani yako cho chote, au kununua cho chote mkononi mwa jirani yako, msidanganyane wenyewe kwa wenyewe;
15 kwa hesabu ya miaka iliyo baada ya yubile, ndivyo utakavyonunua kwa jirani yako, na kama hesabu ya miaka ya mavuno ndivyo atakavyokuuzia wewe.
16 Kama hesabu ya miaka ilivyo ni nyingi ndivyo utakavyoongeza bei yake, na kama hesabu ya miaka ilivyo ni chache ndivyo utakavyopunguza bei yake; kwani yeye akuuzia mavuno kama hesabu yake ilivyo.
17 Wala msidanganyane; lakini utamcha Mungu wako; kwa kuwa mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.
18 Kwa sababu hii zitendeni amri zangu, mkazishike hukumu zangu, na kuzifanya; nanyi mtakaa katika hiyo nchi salama.
19 Nayo nchi itazaa matunda yake, nanyi mtakula na kushiba, na kuketi humo salama.
20 Na kama mkisema, Je! Mwaka wa saba tutakula nini? Angalieni hatutapanda mbegu, wala kukusanya maongeo yetu;
21 ndipo nitawaamria baraka yangu iwe juu yenu mwaka wa sita, nayo utazaa matunda hesabu ya miaka mitatu.
22 Na mwaka wa nane mtapanda mbegu, na kuyala yale matunda, akiba hiyo ya zamani, hata mwaka wa kenda, hata matunda yake yatakapoletwa ndani, mtakula hiyo akiba ya zamani.
23 Nayo nchi haitauzwa kabisa kabisa; kwani nchi ni yangu mimi; maana ninyi ni wageni na wasafiri wangu.
24 Nanyi mtatoa ukombozi kwa ajili ya nchi, katika nchi yote ya milki yenu.
25 Kwamba nduguyo amekuwa maskini, na kuuza sehemu ya milki yake, ndipo jamaa yake aliye karibu naye atakuja, naye ataikomboa ile aliyoiuza nduguye.
26 Na kama mtu hana atakayeikomboa, naye mwenyewe amepata mali na kujiona kuwa anayo ya kutosha kuikomboa;
27 ndipo na aihesabu hiyo miaka ya kuuzwa kwake, na kilichozidi kumrudishia huyo mtu aliyeinunua; naye atairejea milki yake.
28 Lakini asipoweza kujipatia mwenyewe, ndipo hiyo iliyouzwa itakaa mkononi mwake huyo aliyeinunua, hata mwaka wa yubile; na katika yubile itatoka, naye atairejea milki yake.
29 Tena kwamba mtu anauza nyumba ya kukaa, iliyo ndani ya mji wenye kuta, ndipo ana ruhusa kuikomboa katika mwaka mmoja mzima baada ya kuiuza; atakuwa na amri ya kuikomboa muda wa mwaka mzima.
30 Na kama haikukombolewa katika muda wa mwaka mzima, ndipo hiyo nyumba iliyo ndani ya mji wenye kuta itathibitishwa milele kuwa ya huyo aliyeinunua, katika vizazi vyake; nayo haitatoka katika yubile.
31 Lakini nyumba za vijiji, ambavyo havikuzingirwa na kuta, zitahesabiwa pamoja na mashamba ya nchi; nazo zina ruhusa ya kukombolewa, nazo zitatoka katika yubile.
32 Pamoja na hayo, miji ya Walawi, nyumba za miji ya milki yao, Walawi wana ruhusa ya kuzikomboa majira yo yote.
33 Tena kama mtu mmoja wa hao Walawi akikomboa, ndipo nyumba iliyouzwa, na mji wa milki yake, itatoka katika yubile; maana, hizo nyumba za miji ya Walawi ni milki yao kati ya wana wa Israeli.
34 Lakini konde la malisho ya miji yao lisiuzwe kwa kuwa ni milki yao ya daima.
35 Na ikiwa ndugu yako amekuwa maskini, na mkono wake umelegea kwako, ndipo utamsaidia, atakaa nawe kama mgeni, na msafiri.
36 Usitake riba kwake wala faida, bali mche Mungu wako, ili ndugu yako akae nawe.
37 Usimpe fedha yako upate riba, wala usimpe vyakula vyako kwa kujitakia faida.
38 Mimi ndimi Bwana, Mungu wako, niliyewatoa katika nchi ya Misri ili niwape nchi ya Kanaani, nipate kuwa Mungu wenu.
39 Tena kwamba nduguyo amekuwa maskini pamoja nawe, akajiuza kwako; usimtumikishe mfano wa mtumwa;
40 kwako wewe atakuwa mfano wa mtumishi aliyeajiriwa, au mfano wa msafiri; naye atatumika kwako hata mwaka wa yubile;
41 ndipo atakapotoka kwako aende zake, yeye na wanawe pamoja naye, naye atairejea jamaa yake mwenyewe, tena atairejea milki ya baba zake.
42 Kwa kuwa hao ni watumishi wangu, niliowaleta watoke nchi ya Misri; wasiuzwe mfano wa watumwa.
43 Usitawale juu yake kwa nguvu; ila umche Mungu wako.
44 Tena katika habari za watumwa wako na wajakazi wako, utakaokuwa nao; mataifa walio kando-kando yenu, katika hao mtanunua watumwa na wajakazi.
45 Tena katika wana wa wageni wakaao kati yenu mtajinunulia, na katika jamaa zao walio pamoja nanyi, waliowazaa katika nchi yenu; wao watakuwa milki yenu.
46 Nanyi mtawafanya kuwa urithi kwa watoto wenu baada yenu, wawe milki yao; siku zote mtatwaa watumwa wenu katika hao; lakini msitawale kwa nguvu juu ya ndugu zenu, hao wana wa Israeli, wenyewe kwa wenyewe.
47 Tena kama mgeni au mtu akaaye nawe akitajirika, na nduguyo amekuwa maskini karibu naye, akajiuza kwa huyo mgeni, au kwa huyo akaaye kwako, au kwa ukoo wa jamaa ya huyo mgeni;
48 baada ya kuuzwa aweza kukombolewa; mtu mmoja miongoni mwa ndugu zake ana ruhusa kumkomboa;
49 au mjomba wake, au mwana wa mjomba wake, ana ruhusa ya kumkomboa, au mtu awaye yote aliye karibu naye wa jamaa yake, ana ruhusa ya kumkomboa; au kwamba yeye mwenyewe amepata mali, ana ruhusa ya kujikomboa mwenyewe.
50 Naye atafanya hesabu na huyo aliyemnunua, tangu mwaka huo aliojiuza hata mwaka wa yubile; na ile bei ya kuuzwa kwake itakuwa kama hesabu ya hiyo miaka ilivyo; atakuwa pamoja naye kama majira ya mtumishi aliyeajiriwa yalivyo.
51 Kwamba ikali imesalia miaka mingi, kama hesabu yake ilivyo ndivyo atakavyolipa bei ya ukombozi wake, katika hiyo fedha ambayo alinunuliwa kwayo.
52 Tena kwamba imesalia miaka michache tu hata mwaka wa yubile, ndipo atafanya hesabu naye, kama hesabu ya miaka yake ilivyo, ndivyo atakavyolipa tena bei ya ukombozi wake.
53 Kama mtumishi aliyeajiriwa mwaka hata mwaka, ndivyo atakavyokuwa pamoja naye; asitawale juu yake kwa nguvu mbele ya macho yako.
54 Tena kwamba hakukombolewa kwa njia hizi mojawapo, ndipo atatoka katika mwaka wa yubile, yeye, na watoto wake pamoja naye.
55 Kwa kuwa wana wa Israeli ni watumishi; ni watumishi wangu niliowaleta watoke katika nchi ya Misri; mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.