0:00
0:00

Mlango 18

Alipokwisha kusema hayo, Yesu alitoka pamoja na wanafunzi wake kwenda ng'ambo ya kijito Kedroni, palipokuwapo bustani; akaingia yeye na wanafunzi wake.
2 Naye Yuda, yule aliyetaka kumsaliti, alipajua mahali pale; kwa sababu Yesu alikuwa akienda huko mara nyingi pamoja na wanafunzi wake.
3 Basi Yuda, akiisha kupokea kikosi cha askari na watumishi waliotoka kwa wakuu wa makuhani na Mafarisayo, akaenda huko na taa na mienge na silaha.
4 Basi Yesu, hali akijua yote yatakayompata, akatokea, akawaambia, Ni nani mnayemtafuta?
5 Wao wakamjibu, Ni Yesu Mnazareti. Yesu akawaambia, Ni mimi. Yuda naye aliyemsaliti alikuwa amesimama pamoja nao.
6 Basi alipowaambia, Ni mimi, walirudi nyuma, wakaanguka chini.
7 Basi akawauliza tena, Mnamtafuta nani? Wakasema, Yesu Mnazareti.
8 Yesu akajibu, Nimekwisha kuwaambieni ya kwamba ni mimi; basi ikiwa mnanitafuta mimi, waacheni hawa waende zao.
9 Ili litimizwe lile neno alilolisema, Wale ulionipa sikumpoteza hata mmoja wao.
10 Basi Simoni Petro alikuwa na upanga, akaufuta, akampiga mtumwa wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio la kuume. Na yule mtumwa jina lake ni Malko.
11 Basi Yesu akamwambia Petro, Rudisha upanga alani mwake; je! Kikombe alichonipa Baba, mimi nisikinywee?
12 Basi wale askari na yule jemadari na wale watumishi wa Wayahudi walimkamata Yesu, wakamfunga.
13 Wakamchukua kwa Anasi kwanza; maana alikuwa mkwewe Kayafa, yule aliyekuwa Kuhani Mkuu mwaka ule.
14 Naye Kayafa ndiye yule aliyewapa Wayahudi lile shauri ya kwamba yafaa mtu mmoja afe kwa ajili ya watu.
15 Wakamfuata Yesu, Petro na mwanafunzi mwingine. Na mwanafunzi huyo alikuwa amejulikana na Kuhani Mkuu, akaingia pamoja na Yesu katika behewa ya Kuhani Mkuu.
16 Lakini Petro akasimama nje mlangoni. Basi yule mwanafunzi mwingine aliyejulikana na Kuhani Mkuu akatoka, akasema na mngoja mlango, akamleta Petro ndani.
17 Basi yule kijakazi, aliyekuwa mngoja mlango, akamwambia Petro, Wewe nawe, je! Hu mwanafunzi mmojawapo wa mtu huyu? Naye akasema, Si mimi.
18 Na wale watumwa na watumishi walikuwa wakisimama, wamefanya moto wa makaa; maana ilikuwa baridi; wakawa wakikota moto. Petro naye alikuwapo pamoja nao, anakota moto.
19 Basi Kuhani Mkuu akamwuliza Yesu habari za wanafunzi wake, na habari za mafundisho yake.
20 Yesu akamjibu, Mimi nimesema na ulimwengu waziwazi; sikuzote nalifundisha katika sinagogi na katika hekalu, wakusanyikapo Wayahudi wote; wala kwa siri mimi sikusema neno lo lote.
21 Ya nini kuniuliza mimi? Waulize wale waliosikia ni nini niliyowaambia; wao wanajua niliyoyanena.
22 Basi aliposema hayo, mtumishi mmojawapo aliyesimama karibu alimpiga Yesu kofi akisema, Wamjibu hivi Kuhani Mkuu?
23 Yesu akamjibu, Kama nimesema vibaya, ushuhudie ule ubaya; bali kama nimesema vema, wanipigia nini?
24 Basi Anasi akampeleka hali amefungwa kwa Kayafa, Kuhani Mkuu.
25 Na Simoni Petro alikuwa akisimama huko, anakota moto. Basi wakamwambia, Wewe nawe, je! Hu mwanafunzi wake mmojawapo? Naye akakana, akasema, Si mimi.
26 Mtumwa mmojawapo wa Kuhani Mkuu, naye ni jamaa yake yule aliyekatwa sikio na Petro, akasema, Je! Mimi sikukuona wewe bustanini pamoja naye?
27 Basi Petro akakana tena, na mara akawika jimbi.
28 Kisha wakamchukua Yesu kutoka kwa Kayafa mpaka Praitorio, nayo ikawa alfajiri;lakini wao wenyewe hawakuingia ndani ya ile praitorio,wasije wakanajisika,bali wapate kuila Pasaka.
29 Basi Pilato akawatokea nje, akasema, Ni mashitaka gani mnayoleta juu ya mtu huyu?
30 Wakajibu, wakamwambia, Kama huyu asingekuwa mtenda mabaya, tusingemleta kwako.
31 Basi Pilato akawaambia, Haya! Mtwaeni ninyi, mkamhukumu kwa ile torati yenu! Wayahudi wakamwambia, Sisi hatuna ruhusa ya kuua mtu.
32 Ili litimie lile neno lake Yesu alilolisema, akionyesha ni mauti gani atakayokufa.
33 Basi Pilato akaingia tena ndani ya Praitorio, akamwita Yesu, akamwambia, Je! Wewe ni Mfalme wa Wayahudi?
34 Yesu akamjibu, Wewe wasema hivi kwa nafsi yako, au watu wengine walikuambia habari zangu?
35 Pilato akajibu, Ama! Ni Myahudi mimi! Taifa lako na wakuu wa makuhani ndio waliokuleta kwangu. Umefanya nini?
36 Yesu akajibu, Ufalme wangu sio wa ulimwengu huu. Kama ufalme wangu ungekuwa wa ulimwengu huu, watumishi wangu wangenipigania, nisije nikatiwa mikononi mwa Wayahudi. Lakini ufalme wangu sio wa hapa.
37 Basi Pilato akamwambia, Wewe u mfalme basi? Yesu akajibu, Wewe wasema, kwa kuwa mimi ni mfalme. Mimi nimezaliwa kwa ajili ya haya, na kwa ajili ya haya mimi nalikuja ulimwenguni, ili niishuhudie kweli. Kila aliye wa hiyo kweli hunisikia sauti yangu.
38 Pilato akamwambia, Kweli ni nini? Naye akiisha kusema neno hilo akawatokea Wayahudi tena, akawaambia, Mimi sioni hatia yo yote kwake.
39 Lakini kwenu kuna desturi ya mimi kuwafungulia mtu mmoja wakati wa Pasaka; basi, mwapenda niwafungulie Mfalme wa Wayahudi?
40 Basi wakapiga kelele tena kusema, Si huyu, bali Baraba. Naye yule Baraba alikuwa mnyang'anyi.