0:00
0:00

Mlango 14

Naye Hiramu, mfalme wa Tiro, akatuma wajumbe kwa Daudi, akampelekea na mierezi, na waashi, na maseremala, ili wamjengee nyumba.
2 Daudi akajua ya kwamba Bwana amemweka imara ili amiliki juu ya Israeli, kwa kuwa milki yake imeinuka kwa ajili ya watu wake Israeli.
3 Tena Daudi akazidi kuoa wake huko Yerusalemu; akazidi Daudi kuzaa wana na binti.
4 Na haya ndiyo majina ya watoto aliozaliwa huko Yerusalemu; Shamua, na Shobabu, na Nathani, na Sulemani;
5 na Ibhari, na Elishua, na Elpeleti;
6 na Noga, na Nefegi, na Yafia;
7 na Elishama, na Eliada, na Elifeleti.
8 Na waliposikia hao Wafilisti ya kwamba Daudi ametiwa mafuta ili awe mfalme juu ya Israeli wote, Wafilisti wote wakapanda kumtafuta Daudi; naye Daudi akasikia, akatoka nje kupigana nao.
9 Basi hao Wafilisti walikuwa wamekuja na kuteka nyara katika bonde la Warefai.
10 Daudi akamwuliza Mungu, kusema, Je! Nipande juu ya Wafilisti! Utawatia mikononi mwangu? Naye Bwana akamwambia, Panda; kwa kuwa nitawatia mikononi mwako.
11 Basi wakapanda mpaka Baal-perasimu, Daudi naye akawapiga huko; Daudi akasema, Bwana amewafurikia adui zangu kwa mkono wangu, kama mafuriko ya maji. Basi wakapaita mahali pale jina lake Baal-perasimu.
12 Nao wakaiacha miungu yao huko; naye Daudi akaamuru, ikateketezwa kwa moto.
13 Lakini hao Wafilisti wakateka nyara tena mara ya pili bondeni.
14 Na Daudi akamwuliza Mungu tena; naye Mungu akamwambia, Hutapanda kuwafuata; uwageukie mbali, ukawajie huko kuielekea miforsadi.
15 Kisha itakuwa utakapoisikia sauti ya kwenda katika vilele vya miforsadi, ndipo utakapokwenda nje vitani; kwa maana ndipo Mungu ametoka mbele yako, awapige jeshi la Wafilisti.
16 Daudi akafanya kama vile Mungu alivyomwamuru; wakawapiga jeshi la Wafilisti toka Geba mpaka Gezeri.
17 Sifa za Daudi zikafika nchi zote; naye Bwana akawaletea mataifa yote hofu yake.