Mlango 23

Ndipo Ayubu akajibu, na kusema,
2 Hata leo mashitaka yangu yana uchungu; Pigo langu ni zito zaidi ya kuugua kwangu.
3 Laiti ningejua mahali niwezapo kumwona, Nifike hata hapo anapokaa!
4 Ningeiweka daawa yangu mbele yake, Na kukijaza kinywa changu hoja.
5 Ningeyajua maneno atakayonijibu, Na kuelewa na hayo atakayoniambia.
6 Je! Angeshindana nami kwa ukuu wa uwezo wake? La, lakini angenisikiliza.
7 Hapo walekevu wangepata kuhojiana naye; Basi hivyo ningeachiliwa na mwamuzi wangu milele.
8 Tazama, naenda mbele, wala hayuko; Narudi nyuma, lakini siwezi kumwona;
9 Na mkono wa kushoto, afanyapo kazi, lakini siwezi kumwona; Hujificha upande wa kuume, hata nisimwone.
10 Lakini yeye aijua njia niendeayo; Akisha kunijaribu, nitatoka kama dhahabu.
11 Mguu wangu umeshikamana sana na hatua zake; Njia yake nimeishika, wala sikukengeuka.
12 Sikurudi nyuma kuiacha amri ya midomo yake; Nimeyatunza maneno ya kinywa chake zaidi ya riziki yangu,
13 Lakini yeye ni mmoja, ni nani awezaye kumgeuza? Tena nafsi yake ilitakalo, ndilo afanyalo.
14 Kwani yeye hulitimiliza hilo nililoamuriwa; Tena mambo mengi kama hayo ya pamoja naye.
15 Kwa hiyo naona taabu mbele ya uso wake; Nitakapofikiri, namwogopa.
16 Kwani Mungu ameufanya moyo wangu kuzimia, Naye Mwenyezi amenitaabisha;
17 Maana sikufadhaishwa kwa sababu ya giza, Wala kwa sababu giza kuu limenifunika uso.