0:00
0:00

Mlango 6

Ndipo Ayubu akajibu na kusema,
2 Laiti uchungu wangu ungepimwa, Na msiba wangu kutiwa katika mizani pamoja!
3 Kwa kuwa sasa ungekuwa mzito kuliko mchanga wa bahari; Kwa hiyo maneno yangu yamekuwa ya haraka.
4 Kwa kuwa mishale ya huyo Mwenyezi i ndani yangu, Na roho yangu inainywa sumu yake; Vitisho vya Mungu vimejipanga juu yangu.
5 Je! Huyo punda-mwitu hulia akiwa na majani? Au, ng'ombe hulia malishoni?
6 Je! Kitu kisicho na ladha yumkini kulika pasipo chumvi? Au je, uto wa yai una tamu iwayo yote?
7 Roho yangu inakataa hata kuvigusa; Kwangu mimi ni kama chakula kichukizacho.
8 Laiti ningepewa haja yangu, Naye Mungu angenipa neno hilo ninalolitamani sana!
9 Kwamba Mungu angekuwa radhi kuniseta; Kwamba angeulegeza mkono wake na kunikatilia mbali!
10 Hapo ndipo ningefarijika hata sasa; Naam, ningejikuza katika maumivu yasiyoniacha; Kwa kuwa sikuyakana maneno yake Mtakatifu.
11 Nguvu zangu ni zipi, hata ningoje? Na mwisho wangu ni nini, hata nisubiri?
12 Je! Nguvu zangu ni nguvu za mawe? Au mwili wangu, je! Ni shaba?
13 Je! Si kwamba sina msaada ndani yangu. Tena kwamba kufanikiwa kumeondolewa mbali nami?
14 Kwake huyo atakaye kuzima roho inapasa atendewe mema na rafiki; Hata kwake huyo aachaye kumcha Mwenyezi.
15 Ndugu zangu wametenda udanganyifu kama kijito cha maji. Mfano wa fumbi la vijito vipitavyo.
16 Vilivyokuwa vyeusi kwa sababu ya barafu, Ambamo theluji hujificha.
17 Wakati vipatapo moto hutoweka; Kukiwako hari, hukoma mahali pao.
18 Misafara isafiriyo kwa njia yao hugeuka; Hukwea kwenda barani, na kupotea.
19 Misafara ya Tema huvitazama, Majeshi ya Sheba huvingojea.
20 Wametahayari kwa sababu walitumaini; Wakaja huku, nao walifadhaika.
21 Kwani sasa ninyi mmekuwa vivyo; Mwaona jambo la kutisha, mkaogopa.
22 Je! Nilisema, Nipeni? Au, Nitoleeni toleo katika mali yenu?
23 Au, Niokoeni na mkono wa adui? Au, Nikomboeni na mikono ya hao waoneao?
24 Nifunzeni, nami nitanyamaa kimya; Mkanijulishe ni jambo gani nililokosa.
25 Jinsi yafaavyo maneno ya uelekevu! Lakini kuhoji kwenu, je! Kumeonya nini?
26 Je! Mwafikiri kuyakemea maneno? Maana maneno ya huyo aliyekata tamaa ni kama upepo.
27 Naam, mwapenda kuwapigia kura hao mayatima, Na kufanya biashara ya rafiki yenu.
28 Sasa basi iweni radhi kuniangalia; Kwani hakika sitanena uongo usoni penu.
29 Rudini, nawasihi, lisiwe neno la udhalimu; Naam, rudini tena, neno langu ni la haki.
30 Je! Mna udhalimu ulimini mwangu? Je! Makaakaa yangu hayatambui mambo ya madhara?