0:00
0:00

Mlango 101

Rehema na hukumu nitaziimba, Ee Bwana, nitakuimbia zaburi.
2 Nitaiangalia njia ya unyofu; Utakuja kwangu lini? Nitakwenda kwa unyofu wa moyo Ndani ya nyumba yangu.
3 Sitaweka mbele ya macho yangu Neno la uovu. Kazi yao waliopotoka naichukia, Haitaambatana nami.
4 Moyo wa ukaidi utaondoka kwangu, Lililo ovu sitalijua.
5 Amsingiziaye jirani yake kwa siri, Huyo nitamharibu. Mwenye macho ya kiburi na moyo wa majivuno, Huyo sitavumilia naye.
6 Macho yangu yatawaelekea waaminifu katika nchi, Hao wakae nami. Yeye aendaye katika njia kamilifu, Ndiye atakayenitumikia.
7 Hatakaa ndani ya nyumba yangu Mtu atendaye hila. Asemaye uongo hatathibitika Mbele ya macho yangu.
8 Asubuhi hata asubuhi nitawaharibu Wabaya wote wa nchi. Niwatenge wote watendao uovu Na mji wa Bwana.