0:00
0:00

Mlango 92

Ni neno jema kumshukuru Bwana, Na kuliimbia jina lako, Ee Uliye juu.
2 Kuzitangaza rehema zako asubuhi, Na uaminifu wako wakati wa usiku.
3 Kwa chombo chenye nyuzi kumi, Na kwa kinanda, Na kwa mlio wa kinubi.
4 Kwa kuwa umenifurahisha, Bwana, Kwa kazi yako; nitashangilia Kwa ajili ya matendo ya mikono yako.
5 Ee Bwana, jinsi yalivyo makuu matendo yako! Mawazo yako ni mafumbo makubwa.
6 Mtu mjinga hayatambui hayo, Wala mpumbavu hayafahamu.
7 Wasio haki wakichipuka kama majani Na wote watendao maovu wakistawi. Ni kwa kusudi waangamizwe milele;
8 Bali Wewe, Bwana, U Mtukufu hata milele.
9 Maana hao adui zako, Ee Bwana, Hao adui zako watapotea, Na watendao maovu watatawanyika wote pia.
10 Bali pembe yangu umeiinua kama pembe ya nyati, Nimepakwa mafuta mabichi.
11 Na jicho langu limewatazama walioniotea, Sikio langu limesikia habari za waovu walionishambulia.
12 Mwenye haki atasitawi kama mtende, Atakua kama mwerezi wa Lebanoni.
13 Waliopandwa katika nyumba ya Bwana Watasitawi katika nyua za Mungu wetu.
14 Watazaa matunda hadi wakati wa uzee, Watajaa utomvu, watakuwa na ubichi.
15 Watangaze ya kuwa Bwana ni mwenye adili, Mwamba wangu, ndani yake hamna udhalimu.