0:00
0:00

Mlango 22

Mungu wangu, Mungu wangu, Mbona umeniacha? Mbona U mbali na wokovu wangu, Na maneno ya kuugua kwangu?
2 Ee Mungu wangu, nalia mchana lakini hujibu Na wakati wa usiku lakini sipati raha.
3 Na Wewe U Mtakatifu, Uketiye juu ya sifa za Israeli.
4 Baba zetu walikutumaini Wewe, Walitumaini, na Wewe ukawaokoa.
5 Walikulilia Wewe wakaokoka, Walikutumaini wasiaibike.
6 Lakini mimi ni mdudu wala si mtu, Laumu ya wanadamu na mzaha wa watu.
7 Wote wanionao hunicheka sana, Hunifyonya, wakitikisa vichwa vyao;
8 Husema, Umtegemee Bwana; na amponye; Na amwokoe sasa, maana apendezwa naye.
9 Naam, Wewe ndiwe uliyenitoa tumboni, Ulinitumainisha matitini mwa mama yangu.
10 Kwako nalitupwa tangu tumboni, Toka tumboni mwa mamangu ndiwe Mungu wangu.
11 Usiwe mbali nami maana taabu i karibu, Kwa maana hakuna msaidizi.
12 Mafahali wengi wamenizunguka, Walio hodari wa Bashani wamenisonga;
13 Wananifumbulia vinywa vyao, Kama simba apapuraye na kunguruma.
14 Nimemwagika kama maji, Mifupa yangu yote imeteguka, Moyo wangu umekuwa kama nta, Na kuyeyuka ndani ya mtima wangu.
15 Nguvu zangu zimekauka kama gae, Ulimi wangu waambatana na taya zangu; Unaniweka katika mavumbi ya mauti
16 Kwa maana mbwa wamenizunguka; Kusanyiko la waovu wamenisonga; Wamenizua mikono na miguu.
17 Naweza kuihesabu mifupa yangu yote; Wao wananitazama na kunikodolea macho.
18 Wanagawanya nguo zangu, Na vazi langu wanalipigia kura.
19 Nawe, Bwana, usiwe mbali, Ee Nguvu zangu, fanya haraka kunisaidia.
20 Uniponye nafsi yangu na upanga, Mpenzi wangu na nguvu za mbwa.
21 Kinywani mwa simba uniokoe; Naam, toka pembe za nyati umenijibu.
22 Nitalihubiri jina lako kwa ndugu zangu, Katikati ya kusanyiko nitakusifu.
23 Ninyi mnaomcha Bwana, msifuni, Enyi nyote mlio wazao wa Yakobo, mtukuzeni, Mcheni, enyi nyote mlio wazao wa Israeli.
24 Maana hakulidharau teso la mteswa, Wala hakuchukizwa nalo; Wala hakumficha uso wake, Bali alipomlilia akamsikia.
25 Kwako zinatoka sifa zangu Katika kusanyiko kubwa. Nitaziondoa nadhiri zangu Mbele yao wamchao.
26 Wapole watakula na kushiba, Wamtafutao Bwana watamsifu; Mioyo yenu na iishi milele.
27 Miisho yote ya dunia itakumbuka, Na watu watamrejea Bwana; Jamaa zote za mataifa watamsujudia.
28 Maana ufalme una Bwana, Naye ndiye awatawalaye mataifa.
29 Wakwasi wote wa dunia watakula na kusujudu, Humwinamia wote washukao mavumbini; Naam, yeye asiyeweza kujihuisha nafsi yake,
30 Wazao wake watamtumikia. Zitasimuliwa habari za Bwana, Kwa kizazi kitakachokuja,
31 Nao watawahubiri watakaozaliwa haki yake, Ya kwamba ndiye aliyeyafanya.