0:00
0:00

Mlango 19

Mbingu zauhubiri utukufu wa Mungu, Na anga laitangaza kazi ya mikono yake.
2 Mchana husemezana na mchana, Usiku hutolea usiku maarifa.
3 Hakuna lugha wala maneno, Sauti yao haisikilikani.
4 Sauti yao imeenea duniani mwote, Na maneno yao hata miisho ya ulimwengu. Katika hizo ameliwekea jua hema,
5 Kama bwana arusi akitoka chumbani mwake, Lafurahi kama mtu aliye hodari Kwenda mbio katika njia yake.
6 Kutoka kwake lautoka mwisho wa mbingu, Na kuzunguka kwake hata miisho yake, Wala kwa hari yake Hakuna kitu kilichositirika.
7 Sheria ya Bwana ni kamilifu, Huiburudisha nafsi. Ushuhuda wa Bwana ni amini, Humtia mjinga hekima.
8 Maagizo ya Bwana ni ya adili, Huufurahisha moyo. Amri ya Bwana ni safi, Huyatia macho nuru.
9 Kicho cha Bwana ni kitakatifu, Kinadumu milele. Hukumu za Bwana ni kweli, Zina haki kabisa.
10 Ni za kutamanika kuliko dhahabu, Kuliko wingi wa dhahabu safi. Nazo ni tamu kuliko asali, Kuliko sega la asali.
11 Tena mtumishi wako huonywa kwazo, Katika kuzishika kuna thawabu nyingi.
12 Ni nani awezaye kuyatambua makosa yake? Unitakase na mambo ya siri.
13 Umzuie mtumishi wako asitende mambo ya kiburi, Yasinitawale mimi. Ndipo nitakapokuwa kamili, Nami nitakuwa safi, sina kosa lililo kubwa.
14 Maneno ya kinywa changu, Na mawazo ya moyo wangu, Yapate kibali mbele zako, Ee Bwana, Mwamba wangu, na mwokozi wangu.