0:00
0:00

Mlango 84

Maskani zako zapendeza kama nini, Ee Bwana wa majeshi!
2 Nafsi yangu imezionea shauku nyua za Bwana, Naam, na kuzikondea. Moyo wangu na mwili wangu Vinamlilia Mungu aliye hai.
3 Shomoro naye ameona nyumba, Na mbayuwayu amejipatia kioto, Alipoweka makinda yake, Kwenye madhabahu zako, Ee Bwana wa majeshi, Mfalme wangu na Mungu wangu.
4 Heri wakaao nyumbani mwako, Wanakuhimidi daima.
5 Heri ambaye nguvu zake zatoka kwako, Na njia ziendazo Sayuni zimo moyoni mwake.
6 Wakipita kati ya bonde la Vilio, Hulifanya kuwa chemchemi, Naam, mvua ya vuli hulivika baraka
7 Huendelea toka nguvu hata nguvu, Huonekana Sayuni kila mmoja mbele za Mungu.
8 Bwana, Mungu wa majeshi, uyasikie maombi yangu, Ee Mungu wa Yakobo, usikilize,
9 Ee Mungu, ngao yetu, uangalie, Umtazame uso masihi wako.
10 Hakika siku moja katika nyua zako Ni bora kuliko siku elfu. Ningependa kuwa bawabu nyumbani mwa Mungu wangu, Kuliko kukaa katika hema za uovu.
11 Kwa kuwa Bwana, Mungu, ni jua na ngao, Bwana atatoa neema na utukufu. Hatawanyima kitu chema Hao waendao kwa ukamilifu.
12 Ee Bwana wa majeshi, Heri mwanadamu anayekutumaini Wewe.