0:00
0:00

Mlango 24

Yoashi alikuwa na umri wa miaka saba alipoanza kutawala; akatawala miaka arobaini huko Yerusalemu; na jina la mamaye aliitwa Sibia wa Beer-sheba.
2 Yoashi akafanya yaliyo mema machoni pa Bwana siku zote za Yehoyada kuhani.
3 Yehoyada akamwoza wake wawili, naye akazaa wana na binti.
4 Ikawa baada ya haya, Yoashi alikuwa na nia ya kuitengeneza nyumba ya Mungu.
5 Akawakusanya makuhani na Walawi, akawaambia, Nendeni mijini mwa Yuda, mkakusanye katika Israeli wote fedha, ili kuitengeneza nyumba ya Mungu wenu mwaka kwa mwaka, mkafanye bidii kuliharakisha neno hili. Walakini Walawi hawakuliharakisha.
6 Mfalme akamwita Yehoyada mkuu wao, akamwambia, Mbona hukuwataka Walawi waitoze Yuda na Yerusalemu kodi ya Musa mtumishi wa Bwana, na ya kusanyiko la Israeli, kwa ajili ya hema ya ushuhuda?
7 Kwa kuwa wana wa Athalia, yule mwanamke mwovu, walikuwa wameibomoa nyumba ya Mungu; na vitakatifu vyote vya nyumba ya Bwana wamewapatia mabaali.
8 Basi mfalme akaamuru, nao wakafanyiza kasha, wakaliweka nje langoni pa nyumba ya Bwana.
9 Wakapiga mbiu katika Yuda na Yerusalemu, kumletea Bwana kodi aliyoiweka Musa mtumishi wa Mungu, juu ya Israeli jangwani.
10 Wakafurahi maakida wote na watu wote, wakaleta na kutia ndani ya kasha, hata wakaisha.
11 Ikawa wakati walipoletewa kasha wasimamizi wa mfalme kwa mkono wa Walawi, nao wakaona ya kwamba kuna fedha nyingi, huja karani wa mfalme, na msimamizi wake kuhani mkuu, wakatoa yaliyomo kashani, kisha hulichukua kasha, na kulirudisha mahali pake. Ndivyo walivyofanya siku kwa siku, wakakusanya fedha tele.
12 Na mfalme na Yehoyada waliwapa hao waliofanya kazi ya utumishi wa nyumba ya Bwana; nao wakawaajiri waashi na maseremala ili kuitengeza nyumba ya Bwana, na hao pia wafuao chuma na shaba ili kuitengeza nyumba ya Bwana.
13 Hivyo mafundi wakafanya kazi yao, nao wakaimaliza, wakaisimamisha nyumba ya Mungu kama ilivyopasa, wakaifanya imara.
14 Nao walipokwisha, wakaleta mbele ya mfalme na Yehoyada fedha iliyobaki, vikafanyizwa kwayo vyombo vya nyumba ya Bwana, vyombo vya utumishi, navyo vya kutolea, na miiko, na vyombo vya dhahabu na fedha. Wakatoa sadaka za kuteketezwa katika nyumba ya Bwana, daima, siku zote za Yehoyada.
15 Lakini Yehoyada akawa mzee, mwenye umri mwingi, akafa; alipokufa alikuwa na umri wa miaka mia na thelathini.
16 Wakamzika katika mji wa Daudi kati ya wafalme, kwa sababu ametenda mema katika Israeli, na kwa Mungu, na katika nyumba yake.
17 Hata baada ya kufa kwake Yehoyada, wakuu wa Yuda wakamwendea mfalme, wakamsujudia. Naye mfalme akawasikiliza maneno yao.
18 Wakaiacha nyumba ya Bwana, Mungu wa baba zao; wakatumikia maashera na sanamu; ghadhabu ikawajia Yuda na Yerusalemu kwa sababu ya hiyo hatia yao.
19 Hata hivyo akawapelekea manabii, ili kuwarudisha kwa Bwana; nao wakawashuhudia; lakini hawakukubali kuwasikiliza.
20 Na roho ya Mungu ikamjia Zekaria, mwana wa Yehoyada, kuhani; naye akasimama juu ya watu, akawaambia, Mungu asema hivi, Kwani ninyi kuzihalifu amri za Bwana, hata msiweze kufanikiwa? Kwa kuwa mmemwacha Bwana, yeye naye amewaacha ninyi.
21 Basi, wakafanya shauri juu yake, wakampiga kwa mawe kwa amri ya mfalme katika ua wa nyumba ya Bwana.
22 Basi hivyo mfalme Yoashi hakuukumbuka wema, ambao Yehoyada, baba yake, alimfanyia, bali alimwua mwanawe. Naye alipokufa, alisema, Bwana na ayaangalie haya, akayatakie kisasi.
23 Ikawa mwisho wa mwaka, wakakwea juu yake jeshi la Washami; wakafika Yuda na Yerusalemu, wakawaangamiza wakuu wa watu wote miongoni mwa watu, wakamletea mfalme wa Dameski nyara zao zote.
24 Maana wakaja jeshi la Washami watu haba; Bwana akatia mikononi mwao jeshi kubwa mno, kwa sababu wamemwacha Bwana, Mungu wa baba zao. Hivyo wakamfanyia Yoashi hukumu.
25 Hata walipoondoka kwake, (nao walimwacha ameshikwa sana na maradhi,) watumishi wake mwenyewe wakamfanyia fitina kwa ajili ya damu ya mwana wa Yehoyada kuhani, wakamwua kitandani pake, akafa; wakamzika mjini mwa Daudi, lakini hawakumzika katika makaburi ya wafalme.
26 Na hawa ndio waliomfanyia fitina, Zabadi mwana wa Shimeathi mwanamke Mwamoni, na Yehozabadi mwana wa Shimrithi mwanamke Mmoabi.
27 Basi kwa habari ya wanawe, na ukubwa wa mizigo aliolemewa, na majengo ya nyumba ya Mungu, tazama, hayo yameandikwa katika maelezo ya kitabu cha wafalme. Na Amazia mwanawe akatawala mahali pake.