0:00
0:00

Mlango 25

Amazia alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala; akatawala katika Yerusalemu miaka ishirini na kenda; na jina la mamaye aliitwa Yehoadani wa Yerusalemu.
2 Akafanya yaliyo ya adili machoni pa Bwana, lakini si kwa moyo mkamilifu.
3 Basi ikawa, alipopata nguvu katika ufalme wake, akawaua watumishi wale waliomwua mfalme babaye.
4 Lakini watoto wao hakuwaua, ila alifanya sawasawa na hayo yaliyoandikwa katika torati, katika kitabu cha Musa, kama Bwana alivyoamuru, akisema, Mababa wasife kwa makosa ya wana, wala wana wasife kwa makosa ya mababa; lakini kila mtu atakufa kwa dhambi yake mwenyewe.
5 Tena Amazia akawakusanya Yuda, akawaweka sawasawa na nyumba za baba zao chini ya maakida wa maelfu, na maakida wa mamia, naam, Yuda pia, na Benyamini; tangu wenye miaka ishirini na zaidi akawahesabu, akawaona kuwa watu wateule mia tatu elfu, wawezao kwenda vitani, waliozoea mkuki na ngao.
6 Akaajiri pia watu mashujaa mia elfu wa Israeli kwa talanta mia za fedha.
7 Lakini mtu wa Mungu akamjia, akasema, Ee mfalme, usiwaache jeshi la Israeli waende nawe; kwa kuwa Bwana hayupo pamoja na Israeli, yaani, wana wote wa Efraimu.
8 Lakini ukitaka kwenda, haya, jitie nguvu upigane; Mungu atakuangusha mbele ya adui; maana Mungu anazo nguvu za kusaidia, na kuangusha.
9 Amazia akamwambia mtu wa Mungu, Lakini tuzifanyieje zile talanta mia nilizowapa jeshi la Israeli? Mtu wa Mungu akajibu, Bwana aweza kukupa zaidi sana kuliko hizo.
10 Ndipo Amazia akawafarakisha jeshi lililomjia kutoka Efraimu, ili warudi kwao; kwa hiyo ikawaka sana hasira yao juu ya Yuda, nao wakarudi kwao wenye hasira kali.
11 Amazia akapiga moyo konde, akawaongoza watu wake, akaenda mpaka Bonde la Chumvi, akawapiga katika wana wa Seiri watu elfu kumi.
12 Na elfu kumi wengine, ambao wana wa Yuda waliwachukua wali hai, wakawaleta juu ya jabali, wakawaangusha toka juu ya jabali, hata wakavunjika-vunjika wote.
13 Lakini wale watu wa jeshi, aliowarudisha Amazia, wasiende naye vitani, hao wakaiteka miji ya Yuda, tangu Samaria mpaka Beth-horoni, wakawapiga watu elfu tatu, wakachukua nyara nyingi.
14 Basi ikawa, Amazia alipokwisha rudi kutoka kuwaua Waedomi, alileta miungu ya wana wa Seiri, akaisimamisha kuwa miungu yake, akajiinama mbele yao, akaifukizia uvumba.
15 Kwa hiyo hasira ya Bwana ikawaka juu ya Amazia, akampelekea nabii, aliyemwambia, Mbona umeitafuta miungu ya watu, isiyowaokoa watu wao mkononi mwako?
16 Ikawa, aliposema naye, mfalme akamwambia, Je! Tumekutia wewe kuwa mshauri wa mfalme? Nyamaza; kwa nini upigwe? Ndipo yule nabii akaacha, akasema, Najua ya kuwa Mungu amekusudia kukuangamiza, kwa sababu umeyafanya haya, wala hukulisikiliza shauri langu.
17 Ndipo mfalme Amazia akafanya shauri, akatuma wajumbe kwa Yehoashi, mwana wa Yehoahazi mwana wa Yehu,mfalme wa Israeli,kusema,njoo,tutazamane uso kwa uso.
18 Na Yehoashi mfalme wa Israeli akatuma wajumbe kwa Amazia mfalme wa Yuda, kusema, Mbaruti uliokuwako Lebanoni ukatuma kwa mwerezi uliokuwako Lebanoni kusema, Umwoze mwanangu binti yako; kukapita hayawani aliyekuwako Lebanoni, akaukanyaga ule mbaruti.
19 Wasema, Tazama, umewapiga Edomu; na moyo wako wakutukuza ujisifu; kaa nyumbani mwako basi; mbona unataka kujitia bure katika madhara, hata uanguke, wewe na Yuda pamoja nawe?
20 Lakini Amazia hakutaka kusikia, kwa maana hayo yalitoka kwa Mungu, ili awatie mikononi mwao, kwa kuwa wameitafuta miungu ya Edomu.
21 Basi Yehoashi mfalme wa Israeli akakwea; wakatazamana uso kwa uso, yeye na Amazia mfalme wa Yuda huko Beth-shemeshi, ulio wa Yuda.
22 Yuda wakashindwa mbele ya Israeli; wakakimbia kila mtu hemani kwake.
23 Yehoashi mfalme wa Israeli akamtwaa Amazia mfalme wa Yuda, mwana wa Yoashi, mwana wa Ahazia, huko Beth-shemeshi,akamchukua mpaka Yerusalemu ,akauvunja ukuta wa Yerusalemu , toka lango la Efraimu mpaka lango la pembeni ,mikono mia nne.
24 Akaitwaa dhahabu yote, na fedha, na vyombo vyote vilivyoonekana nyumbani mwa Mungu kwa Obed-edomu, na hazina za nyumba ya mfalme, tena watu kuwa amana, akarudi Samaria.
25 Naye Amazia mwana wa Yoashi mfalme wa Yuda, akaishi baada ya kufa kwake Yehoashi mwana wa Yehoahazi, mfalme wa Israeli, miaka kumi na mitano.
26 Na mambo yote ya Amazia yaliyosalia, ya kwanza na ya mwisho, tazama, je! Hayakuandikwa katika kitabu cha wafalme wa Yuda na Israeli?
27 Basi, toka wakati alipogeuka Amazia katika kumfuata Bwana, wakamfanyia fitina katika Yerusalemu; naye akakimbia mpaka Lakishi; lakini wakatuma kumfuata mpaka Lakishi, wakamwua huko.
28 Wakamleta juu ya farasi; wakamzika pamoja na babaze katika mji wa Yuda.