0:00
0:00

Mlango 9

Na malkia wa Sheba aliposikia habari za Sulemani, alikuja ili amjaribu Sulemani kwa maswali ya fumbo huko Yerusalemu, mwenye wafuasi wengi, na ngamia wachukuao manukato, na dhahabu nyingi sana, na vito vya thamani; alipomfikilia Sulemani, akamwambia mambo yote aliyokuwa nayo moyoni mwake.
2 Naye Sulemani akamfumbulia maswali yake yote; wala halikuwako neno alilofichiwa Sulemani, asimwambie.
3 Naye malkia wa Sheba alipoona hekima ya Sulemani, na nyumba aliyoijenga,
4 na vyakula vya mezani mwake, na kikao cha watumishi wake, na usimamizi wao wangoje wake, na mavazi yao; na wanyweshaji wake, na mavazi yao; na daraja yake ya kupandia mpaka nyumba ya Bwana; roho yake ilizimia.
5 Akamwambia mfalme, Ndizo kweli habari zile nilizozisikia katika nchi yangu za mambo yako na za hekima yako.
6 Lakini mimi sikuyasadiki maneno yao, hata nilipokuja na kuona kwa macho yangu; wala, tazama, ukuu wa hekima yako sikuambiwa nusu; wewe umezidi kuliko habari nilizozisikia.
7 Heri watu wako, na heri hawa watumishi wako, wasimamao mbele yako sikuzote, wakisikia hekima yako.
8 Na ahimidiwe Bwana, Mungu wako, aliyependezwa nawe, ili akuweke juu ya kiti chake cha enzi, kuwa mfalme wake Bwana, Mungu wako; kwa kuwa Mungu wako amewapenda Israeli, kuwathibitisha milele, kwa hiyo amekufanya kuwa mfalme juu yao, ufanye hukumu na haki.
9 Basi akampa mfalme talanta mia na ishirini za dhahabu, na manukato mengi mengi sana, na vito vya thamani; wala haukuja wingi wa manukato, kama hayo aliyopewa mfalme Sulemani na malkia wa Sheba.
10 Tena watumishi wa Hiramu, pamoja na watumishi wa Sulemani, walioleta dhahabu kutoka Ofiri, wakaleta miti ya msandali, na vito vya thamani.
11 Mfalme akayafanya kwa miti hiyo ya msandali madari ya nyumba ya Bwana, na nyumba ya mfalme, na vinubi na vinanda vya hao waimbaji; wala haijatokea kama hiyo katika nchi ya Yuda.
12 Mfalme Sulemani akampa malkia wa Sheba haja yake yote, kila alilotaka, zaidi ya vile alivyomletea mfalme. Basi akarudi, akaenda zake katika nchi yake, yeye na watumishi wake.
13 Basi uzani wa dhahabu iliyomfikia Sulemani mwaka mmoja, ndio talanta mia sita sitini na sita za dhahabu;
14 mbali na ile waliyoileta wachuuzi na wafanya biashara; tena wafalme wote wa Arabuni, na maliwali wa nchi wakamletea Sulemani dhahabu na fedha.
15 Mfalme Sulemani akafanya ngao mia mbili za dhahabu iliyofuliwa; ngao moja hupata shekeli mia sita za dhahabu iliyofuliwa.
16 Na vigao mia tatu vya dhahabu iliyofuliwa; kigao kimoja hupata shekeli mia tatu za dhahabu; mfalme akaviweka katika nyumba ya mwitu wa Lebanoni.
17 Tena mfalme akafanya kiti cha enzi kikubwa cha pembe, akakifunikiza kwa dhahabu iliyo safi.
18 Kiti kile kilikuwa na daraja sita, tena na kikao cha miguu cha dhahabu, navyo vilikuwa vimeshikamana na kiti; na mikono huko na huko mahali pa kuketi, na simba wawili wakisimama kando ya hiyo mikono.
19 Na simba kumi na wawili wamesimama juu ya daraja sita, huko na huko; wala hakikufanyika kwa mfano wake katika ufalme wo wote.
20 Na vyombo vyote vya kunywea vya mfalme Sulemani vilikuwa vya dhahabu, na vyombo vyote vya nyumba ya mwitu wa Lebanoni vilikuwa vya dhahabu iliyosafika; fedha haikuhesabiwa kuwa kitu siku za Sulemani.
21 Kwa kuwa mfalme alikuwa na merikebu zilizokwenda Tarshishi pamoja na watumishi wa Hiramu; mara moja katika miaka mitatu huja merikebu za Tarshishi, zikileta dhahabu, na fedha, na pembe, na nyani, na tausi.
22 Basi mfalme Sulemani akawapita wafalme wote wa duniani kwa mali, na kwa hekima.
23 Wafalme wote wa duniani wakamtafuta Sulemani uso wake, ili waisikie hekima yake, Mungu aliyomtia moyoni.
24 Wakaleta kila mtu zawadi yake, vyombo vya fedha, na vyombo vya dhahabu, na mavazi, na silaha, na manukato, na farasi, na nyumbu, hesabu yake ya mwaka kwa mwaka.
25 Sulemani akawa na mazizi ya farasi na magari elfu nne, na wapandao farasi kumi na mbili elfu, aliowaweka katika miji ya magari, na pamoja na mfalme huko Yerusalemu.
26 Akatawala juu ya wafalme wote toka Mto hata nchi ya Wafilisti, na hata mpaka wa Misri.
27 Mfalme akafanya fedha humo Yerusalemu kuwa kama mawe, na mierezi akaifanya kuwa kama mikuyu iliyomo Shefela, kwa kuwa mingi.
28 Wakamletea Sulemani farasi kutoka Misri, na kutoka nchi zote.
29 Basi mambo yake Sulemani yaliyosalia, ya kwanza, na ya mwisho, je! Hayakuandikwa katika tarehe ya Nathani nabii, katika unabii wa Ahiya, Mshiloni, na katika maono ya Ido mwonaji juu ya Yeroboamu mwana wa Nebati?
30 Akatawala Sulemani katika Yerusalemu juu ya Israeli wote miaka arobaini.
31 Naye Sulemani akalala na baba zake, akazikwa mjini mwa Daudi babaye; akatawala Rehoboamu mwanawe badala yake.