0:00
0:00

Mlango 29

Hezekia alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala; akatawala katika Yerusalemu miaka ishirini na kenda; na jina la mamaye aliitwa Abiya binti Zekaria.
2 Akafanya yaliyo ya adili machoni pa Bwana, sawasawa na yote aliyoyafanya Daudi babaye.
3 Yeye, katika mwaka wa kwanza wa kutawala kwake, katika mwezi wa kwanza, aliifungua milango ya nyumba ya Bwana, akaitengeneza.
4 Akawaingiza makuhani na Walawi, akawakusanya uwandani upande wa mashariki,
5 akawaambia, Nisikieni, enyi Walawi; jitakaseni nafsi zenu sasa, mkaitakase na nyumba ya Bwana, Mungu wa baba zenu, mkautoe uchafu katika patakatifu.
6 Kwa maana baba zetu wameasi, na kufanya yaliyo maovu machoni pa Bwana, Mungu wetu, wamemwacha, na kugeuzia mbali nyuso zao na makao ya Bwana, na kumpa maungo.
7 Tena wameifunga milango ya ukumbi, na kuzizima taa, wala hawakufukiza uvumba, wala hawakumtolea Mungu wa Israeli sadaka za kuteketezwa katika patakatifu.
8 Kwa hiyo hasira ya Bwana imekuwa juu ya Yuda na Yerusalemu, naye amewatoa kuwa matetemeko, wawe ushangao, na mazomeo, kama mwonavyo kwa macho yenu.
9 Kwa kuwa, tazama, baba zetu wameangamia kwa upanga, na wana wetu, na binti zetu, na wake zetu wametekwa kwa ajili ya hayo.
10 Basi nia yangu ni kufanya agano na Bwana, Mungu wa Israeli, ili kwamba hasira yake kali itugeukie mbali.
11 Basi wanangu, msijipurukushe sasa, kwa kuwa Bwana amewachagua ninyi msimame mbele yake, kumhudumia, nanyi mpate kuwa watumishi wake, mkafukize uvumba.
12 Ndipo wakaondoka Walawi, Mahathi mwana wa Amasai, na Yoeli mwana wa Azaria, wa wana wa Wakohathi; na wa wana wa Merari, Kishi mwana wa Abdi, na Azaria mwana wa Yehaleleli; na wa Wagershoni, Yoa mwana wa Zima na Edeni mwana wa Yoa;
13 na wa wana wa Elisafani, Shimri na Yeueli; na wa wana wa Asafu, Zekaria na Matania;
14 na wa wana wa Hemani, Yehueli na Shimei; na wa wana wa Yeduthuni, Shemaya na Uzieli.
15 Wakawakusanya ndugu zao, wakajitakasa, wakaingia, kama alivyoamuru mfalme kwa maneno ya Bwana, ili waisafishe nyumba ya Bwana.
16 Nao makuhani wakaingia nyumbani mwa Bwana, katika mahali pa ndani, ili waisafishe, wakatoa uchafu wote waliouona hekaluni mwa Bwana, wakautupa nje uani mwa nyumba ya Bwana. Walawi wakautwaa, ili wauchukue nje mpaka kijito cha Kidroni.
17 Basi wakaanza kutakasa siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza, hata siku ya nane ya mwezi wakafika katika ukumbi wa Bwana; wakaitakasa nyumba ya Bwana katika muda wa siku nane; wakamaliza siku ya kumi na sita ya mwezi wa kwanza.
18 Wakaingia ndani kwa Hezekia mfalme, wakasema, Tumeisafisha nyumba yote ya Bwana, na madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, pamoja na vyombo vyake vyote, na meza ya mikate ya wonyesho, pamoja na vyombo vyake vyote.
19 Tena vyombo vyote alivyovitupa mfalme Ahazi alipotawala, hapo alipoasi, tumevitengeza na kuvitakasa; navyo, tazama, vipo mbele ya madhabahu ya Bwana.
20 Ndipo Hezekia mfalme akaamka mapema, akakusanya wakuu wa mji, akapanda nyumbani kwa Bwana.
21 Wakaleta ng'ombe waume saba, na kondoo waume saba, na wana-kondoo saba, na mabeberu saba, kuwa sadaka ya dhambi kwa ajili ya ufalme, na kwa ajili ya patakatifu, na kwa ajili ya Yuda. Akaamuru makuhani, wana wa Haruni, wawatoe madhabahuni pa Bwana.
22 Basi wakawachinja ng'ombe, na makuhani wakaipokea damu, wakainyunyiza madhabahuni; wakawachinja kondoo waume, na kuinyunyiza damu madhabahuni; wakawachinja na wana-kondoo, na kuinyunyiza damu madhabahuni.
23 Wakawaleta karibu mabeberu wa sadaka ya dhambi mbele ya mfalme na kusanyiko; wakawawekea mikono yao;
24 na makuhani wakawachinja, wakaitoa damu yao kuwa sadaka ya dhambi madhabahuni, ili kuwafanyia Israeli wote upatanisho; maana mfalme aliamuru Israeli wote wafanyiwe sadaka ya kuteketezwa na sadaka ya dhambi.
25 Akawasimamisha Walawi nyumbani mwa Bwana wenye matoazi, wenye vinanda, na wenye vinubi, kama alivyoamuru Daudi, na Gadi mwonaji wa mfalme, na Nathani nabii; kwani Bwana aliamuru hivi kwa manabii wake.
26 Wakasimama Walawi wenye vinanda vya Daudi, na makuhani wenye mapanda.
27 Hezekia akaamuru kutoa sadaka ya kuteketezwa madhabahuni. Na wakati ilipoanza sadaka hiyo ya kuteketezwa, ukaanza na huo wimbo wa Bwana, na mapanda, pamoja na vinanda vya Daudi mfalme wa Israeli.
28 Na kusanyiko lote wakaabudu, waimbaji wakaimba, wenye mapanda wakapiga; haya yote yakaendelea hata ilipomalizika sadaka ya kuteketezwa.
29 Hata walipokwisha kutoa sadaka, mfalme, na hao wote waliokuwapo naye, wakasujudia, wakaabudu.
30 Tena Hezekia mfalme na wakuu wakawaamuru Walawi, wamwimbie Bwana sifa kwa maneno ya Daudi, na ya Asafu mwonaji. Wakaimba sifa kwa furaha, wakainama vichwa, wakaabudu.
31 Ndipo Hezekia akajibu, akasema, Sasa mmejifanya wakfu kwa Bwana, karibuni mkalete dhabihu na matoleo ya shukrani nyumbani mwa Bwana. Basi kusanyiko wakaleta dhabihu na matoleo ya shukrani; na wote wenye moyo wa ukarimu, wakaleta sadaka za kuteketezwa.
32 Na hesabu ya sadaka hizo za kuteketezwa walizozileta kusanyiko ikawa ng'ombe waume sabini, kondoo waume mia, na wana-kondoo mia mbili; hao wote walikuwa ni sadaka ya kuteketezwa kwa Bwana.
33 Na vitu vitakatifu vilikuwa ng'ombe mia sita, na kondoo elfu tatu.
34 Lakini makuhani walikuwa wachache, wasiweze kuchuna sadaka zote za kuteketezwa; basi ndugu zao Walawi wakawasaidia, hata ilipokwisha kazi, na hata makuhani walipojitakasa; kwa kuwa Walawi walikuwa wenye mioyo ya adili kwa kujitakasa kuliko makuhani.
35 Na tena sadaka za kuteketezwa nazo zilikuwa nyingi, pamoja na mafuta ya sadaka za amani, na sadaka za kinywaji kwa kila sadaka ya kuteketezwa. Hivyo ikatengezeka huduma ya nyumba ya Bwana.
36 Akafurahi Hezekia, na watu wote, kwa sababu ya hayo Mungu aliyowatengenezea watu; maana jambo hilo likawa kwa ghafula.