0:00
0:00

Mlango 31

Ole wao watelemkao kwenda Misri wapate msaada, na kutegemea farasi; watumainio magari kwa kuwa ni mengi, na wapanda farasi kwa kuwa ni hodari sana; lakini hawamwangalii Mtakatifu wa Israeli, wala hawamtafuti Bwana!
2 Lakini yeye naye ana akili, naye ataleta uovu, wala hatayatangua maneno yake; bali ataondoka juu ya nyumba yao watendao mabaya, na juu ya msaada wa hao watendao maovu.
3 Basi Wamisri ni wanadamu wala si Mungu, na farasi zao ni nyama wala si roho; na Bwana atakaponyosha mkono wake, yeye asaidiaye atajikwaa, na yeye asaidiwaye ataanguka, nao wote pamoja watakoma.
4 Maana Bwana aniambia hivi, Kama vile ilivyo simba angurumapo na mwana-simba juu ya mawindo yake, wachungaji wengi wakiitwa ili kumpiga, lakini hatiwi hofu na sauti zao, wala kufanya woga kwa sababu ya mshindo wao; ndivyo Bwana wa majeshi atakavyoshuka ili kufanya vita juu ya mlima Sayuni, na juu ya kilima chake.
5 Kama ndege warukao, Bwana wa majeshi ataulinda Yerusalemu; ataulinda na kuuokoa, atapita juu yake na kuuhifadhi.
6 Mwelekeeni yeye mliyemwasi sana, enyi wana wa Israeli.
7 Maana katika siku hiyo kila mtu atatupa sanamu zake za fedha, na sanamu zake za dhahabu, ambazo mikono yenu imezifanya, zikawa dhambi kwenu.
8 Ndipo huyo Mwashuri ataanguka kwa upanga ambao si wa mtu; na upanga usio upanga wa mtu utamla; naye ataukimbia upanga, na vijana wake watatoa kodi.
9 Na mwamba wake utatoweka kwa sababu ya hofu, nao wakuu wake wataionea bendera hofu kuu, asema Bwana, ambaye moto wake u katika Sayuni, na tanuru yake katika Yerusalemu.